April 28, 2014





Na Saleh Ally
NOVEMBA 29, 1987, Kocha Alex Ferguson alipiga hodi nyumbani kwao Ryan Giggs ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 14. Kazi ilikuwa ni moja tu, kumshawishi mzazi wa mchezaji huyo.

Ferguson alitaka kumshawishi mama Giggs kwamba mwanaye ahame kutoka katika timu ya watoto ya Manchester City na kujiunga na ile ya Manchester United ambayo ndiyo alikuwa ameifundisha kwa mwaka mmoja tu tangu ajiunge nayo akitokea Aberdeen.

Uamuzi huo ulitokana na Giggs kufunga mabao matatu ‘hat trick’ katika mechi ya timu yake ya watoto chini ya miaka 15 ya Salford Boys dhidi ya Manchester United. Ferguson akamchukua mtaalamu wa vipaji Joe Brown na kuongozana naye hadi kwao kumshawishi mama yake.
Wakati Ferguson akifanya kazi ya kumshawishi mama Giggs, mshambuliaji nyota wa Manchester United, Wayne Rooney alikuwa na umri wa miaka miwili. Sasa wawili hao wamepita hatua mbili za maisha, mchezaji na mwenzake na sasa mchezaji na kocha wake!

Hii inaonyesha dunia ya soka ina mengi lakini kivutio zaidi, kwani Giggs leo amechukua nafasi ya Ferguson ambaye wakati huo alivutiwa naye kama mchezaji na kwenda kumshawishi ajiunge na Man United ambayo ameichezea mechi 962, si mchezo.
Gumzo ni kufukuzwa kwa Kocha David Moyes aliyerithi nafasi ya Ferguson halafu akaboronga kupindukia, sasa amepewa Giggs ambaye ni kocha wa muda lakini ameanza kazi vizuri kwa ushindi wa mabao 4-0 na Rooney akipiga mabao mawili.

Giggs amepewa ukocha wa muda, anayetarajiwa kuchukua nafasi hiyo ni Louis van Gaal raia wa Uholanzi. Lakini mjadala uko hivi, kwamba Giggs anaweza kuendelea kuwa kocha wa Manchester na kuifanya iendelee kushinda?
Maana anaweza kuifanya icheze kwa staili ile ya Ferguson ambayo Wa-man United wanaona ndiyo sahihi, tena kitu kizuri kwenye benchi la ufundi yuko na Manchester wa kweli waliopewa jina la “Class of 92” ambao ni Paul Scholes, Phil Neville na Nicky Butt.

Class of 92 kuiongoza Man United, unaweza kusema inaongozwa na vijana au watoto wa Ferguson ambao hakuna ubishi kwa asilimia zaidi ya 60, watatumia mbinu au mifumo iliyokuwa akiitumia kocha huyo wakati akiwafundisha tokea timu za chini hadi timu kubwa wakiwa makinda hadi walipofikia kuitwa wakongwe na wengine wakaondoka.

Kumbuka Ferguson aliwahi kumtandika Giggs kofi mbele ya mpenzi wake pamoja na wenzake wakiwemo Scholes, Neville, Butt na David Beckham, Giggs alipowaalika wenzake hao kwake na kelele za muziki zikawaudhi majirani ambao walimpigia kocha huyo na kumueleza “watoto wako wanatubughudhi”.

Maana yake Giggs anaijua zaidi kazi ya Ferguson ambaye amefanya naye kazi kwa zaidi ya miaka 20, lakini ana watu wanaomsaidia na wanaoijua Man United. Wanaoweza kufanya mambo yaende vizuri.

Sahihi kumuacha Giggs aendelee baada ya kushinda mechi moja iliyozaa mabao manne na pointi tatu? Kama wakimuachia timu, litakuwa ni kosa moja, tena kubwa, hilo ndilo jibu.
Si kwamba Norwich ni dhaifu hapana, lakini Man United ni kubwa kumuachia Giggs katika kipindi hiki. Badala yake anatakiwa kocha mwenye jina kubwa, uwezo na uzoefu zaidi mfano wa van Gaal.

Kuwa na mtu kama van Gaal, bado kutaongeza heshima na mvuto wa Man United na kusaidia wachezaji wengine nyota kutoka sehemu mbalimbali kuamini Man United ni sehemu sahihi ya kwenda ambayo wanaweza kufanya kazi.
Kumuacha Giggs awe kocha kutajenga hofu na ikitokea akakosea na kutimuliwa, pia kutajenga hofu kwa wenzake hasa Class of 92 ambao kuwapunguza morali kipindi hiki ni sawa na kuitupia United kaburini. Lakini ni vizuri kutomuondoa Giggs katika nafasi ya kocha msaidizi.
Moyes alikosea kuliondoa benchi lote la ufundi lililokuwa chini ya Ferguson na kuleta watu wake, kama van Gaal akipata kazi, asifanye kosa kama hilo kwa kuwa anamhitaji Giggs na Class of 92. Hawawezi kumshinda kwa kuwa aliwahi kuwa bosi wa Jose Mourinho wakiwa Barcelona na wakafanya kazi vizuri kabisa.

Giggs amekuwa kocha ambaye ameweka rekodi mbili za haraka siku chache tu baada ya kuchukua nafasi yake hiyo kwa muda.
Moja ni kuonyesha anapendwa zaidi kuliko kocha mwingine yeyote baada ya makocha wawili waliokaa muda mrefu zaidi ambao ni Ferguson na Matt Busby aliyeifundisha Man United kuanzia Oktoba Mosi 1945 hadi Juni 4, 1969, kabla ya kurudi na kuinoa kwa mwaka mmoja na ukawa ndiyo mwisho wake na United.
Rekodi ya pili aliyoweka Giggs ni kuwa mtu wa kwanza mwenye asili ya Bara la Afrika kuinoa klabu hiyo, haijawahi kutokea.
Asili ya Giggs ni nchini Sierra Leone barani Afrika ingawa mama yake ni raia wa Wales na kwa kuwa alizaliwa nchini humo, moja kwa moja amekuwa raia wa huko.
Wakati akiwa mwanafunzi, Giggs ni kati ya wachezaji ambao wamesimulia mengi mabaya waliyokutana nayo kutokana na ubaguzi wa rangi ingawa umaarufu na muonekano wake umekuwa si rahisi watu wengi kugundua kuwa ana asili ya Afrika ambako mpira umezaliwa.


Kombe la Dunia la Klabu (1): 2008

REKODI ZA GIGGS NA PREMIER LEAGUE
•Ana rekodi ya kubeba makombe yote 13 iliyoshinda Man United wakati wa Ferguson.
•Amecheza mechi nyingi zaidi za ligi hiyo kuliko mwingine, amecheza mechi  611.
•Ndiye mchezaji aliyetoa pasi nyingi zaidi zilizozaa mabao katika ligi hiyo.
•Mchezaji pekee aliyecheza misimu 22 mfululizo ya ligi hiyo bila kukosa hata mmoja.
•Mchezaji pekee aliyefunga mabao katika ligi ya Premiership kwa misimu 21 mfululizo.
•Mchezaji aliyeanza mechi 794 za kikosi cha kwanza cha United.
•Mchezaji wa kwanza kufunga mabao 100 kwa Man United.
•Kiungo wa pili kufunga mabao 100 Premiership baada ya Matt Le Tissier.

REKODI ZA GIGGS NA LIGI YA MABINGWA:
•Amecheza misimu 17 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia akiwa amecheza misimu 11 mfululizo. Anazidiwa na Raul Gonzalez tu aliyecheza mfululizo mara 14.
•Mwingereza aliyecheza mechi nyingi zaidi za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
•Akiwa na umri wa miaka 37 na siku 289, aliweka rekodi ya kuwa mkongwe kufunga bao Ligi ya Mabingwa Ulaya, Man United ilipocheza na Benfica, Septemba 14, 2011.

MAKOMBE YA GIGGS NA UNITED:
Premier League (13): 1992–93, 1993–94, 1995–96, 1996–97, 1998–99, 1999–2000, 2000–01, 2002–03, 2006–07, 2007–08, 2008–09, 2010–11, 2012–13
Kombe FA (4): 1993–94, 1995–96, 1998–99, 2003–04
Kombe la Ligi: (4): 1991–92, 2005–06, 2008–09, 2009–10
Ngao ya Jamii ya (9): 1993, 1994, 1996, 1997, 2003, 2007, 2008, 2010, 2013
Ligi ya Mabingwa Ulaya (2): 1998–99, 2007–08
Super Cup ya Uefa (1): 1991
Kombe la Intercontinental (1): 1999

Rekodi ya Class of 92 wanaoiongoza Man United sasa:
Phil Neville – Alijiunga United 1992
Mechi: 386

Makombe:
Ligi ya Mabingwa (1)
Premier League (6)
Kombe la FA (3)

Nicky Butt - Alijiunga United 1991
Mechi: 387

Makombe:
Ligi ya Mabingwa (1)
Premier League (6)
Kombe la FA (3)
 
Paul Scholes - Alijiunga United 1991
Mechi: 718

Makombe:
Ligi ya Mabingwa (2)
Premier League (11)
Kombe la FA (3)
Kombe la Ligi (2)

Ryan Giggs - Alijiunga United 1987
Mechi: 962

Makombe:
Ligi ya Mabingwa (2)
Premier League (13)
Kombe la FA (4)
Kombe la Ligi (4)

Fin.




1 COMMENTS:

  1. Hapana, siyo kweli, Giggs siyo Mwafrika at all, give us proof, don't give us cheaper stories without any proof.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic