Uwanja wa Azam Complex unaomilikiwa na Azam FC, umepata bahati
baada ya kuchaguliwa na Kampuni ya Airtel Tanzania kwa ajili ya kuendesha kliniki
ya soka ya kimataifa ya Manchester United, kuanzia Aprili 23 mpaka 27, mwaka
huu.
Hii ni mara ya pili kwa kliniki kama hiyo kufanyika hapa nchini,
kufuatia kliniki kama hii iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa mwaka 2011.
Kliniki hiyo ina nia ya kuwaendeleza vijana waliofanya vizuri kwenye
michuano ya mwaka jana iliyofanyika Lagos, Nigeria na kushirikisha nchi 12
ambapo timu ya Tanzania ya wasichana ilitwaa ubingwa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano amesema
hiyo ni sehemu ya mpango kabambe wa Airtel kusaka na kuendeleza vipaji vya soka
Tanzania na Afrika kwa jumla.
“Airtel inajivunia kuwekeza kwenye soka, mchezo ambao una uwezo wa
kuileta jamii pamoja kupitia hamasa ya mashabiki na yenye uwezo wa kuwafanya
wachezaji kupata elimu pamoja na ajira,” alisema Singano.
Aliongeza kuwa Airtel inajivunia programu ya Airtel Rising Stars kwa
kuleta furaha na hamasa kubwa miongoni mwa vijana wa Tanzania, hivyo kuifanya Kampuni
ya Airtel kuhamasika kuendelea kuwekeza kwenye soka.
Upande wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine
Mwesigwa, aliishukuru Airtel kwa mpango huo makini wenye nia ya kutafuta na
kuendeleza vipaji chipukizi vya soka Tanzania.
Washiriki wa kliniki hii watatoka nchi za Kenya, Uganda, Malawi, Chad,
Burkina Faso, Sierra Leon, Shelisheli, Congo Brazzaville, Nigeria, Zambia na
wenyeji Tanzania ambao watawakilishwa na wachezaji 19.
0 COMMENTS:
Post a Comment