July 30, 2014



Na Saleh Ally
TOKEA enzi za kocha Alex Ferguson, Manchester United ilionyesha kuvutiwa kwa kiasi kikubwa na kazi ya kiungo wa Athletic Bilbao ya Hispania. Juhudi zao za kumnasa pamoja na kwamba walitoa dau zuri, zikakwama.


Manchester United ilitoa dau la pauni milioni 24 (zaidi ya Sh bilioni 67) kumnasa Ander Herrera Aguera, lakini bado Bilbao wakakataa kumuachia. Haikuishia hapo, United iliendelea kumfuatilia kwa juhudi kubwa hadi ilipomnasa msimu huu kwa dau la pauni milioni 29.

Huenda wengi walishangazwa na juhudi hizo za Manchester United kutaka kumnasa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 sasa. Ana nini, labda sababu ni ipi?

Mwisho wamefanikiwa kumpata na imegundulika Barcelona pia ilikuwa ikifanya juhudi za chinichini kumnasa Herrera lakini kiungo huyo alikuwa na ndoto siku moja aichezee Real Madrid.


Tayari yuko Manchester United na katika mechi chache tu alizocheza za kirafiki akiwa chini ya Louis van Gaal huko Marekani, kiungo huyo ameonyesha kweli anastahili kuitumikia timu hiyo.

Swali, anaweza kuwa suluhisho la matatizo ya kiungo? Uwezo mkubwa alionao Herrera kucheza kama kiungo wa ulinzi au kiungo mgawaji, mchezeshaji kweli unaweza kumaliza tatizo kubwa la kiungo lililoonekana msimu uliopita?

Van Gaal ana nafasi ya kuchagua anataka amchezeshe sehemu ipi, lakini ameonyesha ana uwezo mkubwa wa kukaba na kilichoelezwa kuwa uchezaji wake ni staili ya Kiingereza badala ya Kihispania kweli kimeonekana.

Kwa muda mfupi amejichanganya na wachezaji wa Manchester na kuonekana kama amekuwa nao kwa muda mrefu. Kizuri zaidi, hata wachezaji wengine wa United wameonyesha kumkubali, ni dalili njema kwamba watataka kumsaidia ili awe msaada kwenye timu.

Ujio wake unaweza kuwa raha kwa wengine na chachu kwa baadhi kama Marouane Fellaini ambaye huenda atalazimika kuondoka kwa kuwa hakuwa na msimu mzuri tangu alipotua United akitokea Everton.

Takwimu zinaonyesha anaweza kuwa dawa mpya ya matatizo ya Manchester United kwenye safu ya kiungo ingawa wapo wenye hofu kwamba kuna viungo walitoka kwenye timu zao wakionekana ni msaada, wakafeli baada ya kutua United.

Takwimu zinaonyesha katika maisha yake ya soka la kulipwa kuanzia akiwa Zaragoza B, msimu wa 2008-09, Herrera amecheza jumla ya mechi 229, amefunga mabao 19 tu.

Ingawa ameshaonyesha ana uwezo wa kufunga, lakini United inamtaka kwa ajili ya uunganishaji wa timu, hivyo haiwezi kuwa na hofu na suala la ufungaji kwa kuwa wenye uwezo wa kufanya hivyo inao wengi.

Mechi 186 za La Liga akiwa amefunga mabao 15, zinaonyesha ana uzoefu wa kutosha na hatakwenda kufundishwa nini cha kufanya.

Msimu uliopita alimaliza La Liga akiwa na wastani wa pasi 47, alitengeneza nafasi 53 safi za kusaidia kufunga lakini tano ndiyo zikazaa mabao. Tatizo lake kubwa ni faulo, msimu huo wa 2013-14 alifanya faulo 46 lakini akalambwa kadi 7 tu za njano.

Tatizo jingine alilonalo ni kwamba, kama mchezo ‘ukichafuka’, watu wakaanza kucheza kibabe, yeye huwa hautulizi, badala yake anauchafua zaidi, kiaina unaweza kusema ni mbabe.

Uwezo wake umefanya wachambuzi wengi kumuweka kwenye daraja la wachezaji nyota kwenye kiungo kama Andres Iniesta (Barcelona), Mesut Ozil (Arsenal) na Cesc Fabregas (Barca/sasa Chelsea).

Angalia takwimu za msimu uliopita za Herrera, Ozil, Fabregas na Iniesta.
 
                                 PASI           ASILIMIA                   PASI ZA MABAO     MABAO       MECHI     DAKIKA



Ferrera          47               80.6%                       5                      5                  33             2,548

Iniesta           63                90.7%                       7                     3                   35           2,488

Fabregas        60                87%                       13                     8                    36           2,463

Ozil               63                 88%                        9                      5                    26          2,149



  


FIN.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic