March 18, 2016



Na Saleh Ally
MMOJA wa viungo bora kabisa katika kipindi hiki ambao wanacheza katika kiwango cha Ligi Kuu Tanzania Bara ni Salum Abubakary, maarufu kama Sure Boy.

Sure Boy kwa muonekano, umbo lake ni dogo sana lakini ni kati ya wachezaji ambao wanathibitisha ule msemo wa anayejua baiskeli, kawaida huwa anajua tu.

Uchezaji wake ni wa uhakika, ana uwezo mkubwa kuficha au kumiliki mpira, pasi za uhakika na pia amekuwa akifunga moja ya mabao bora kabisa. Moja ambalo ni mfano mzuri ni lile dhidi ya Bidvest ya Afrika Kusini ambapo Azam FC ilishinda kwa mabao 3-0 ikiwa ugenini jijini Johannesburg na Sure Boy akatungua shuti la kutosha kuandika bao hilo.

Katika mahojiano na Sure Boy ambaye ni mtoto wa winga nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Abubakary Salum ‘Sure Boy’, kuhusiana na mambo mbalimbali ya maendeleo ya soka ikiwa ni pamoja na ndoto zake za kucheza soka nje ya Tanzania. Kiungo huyo, bado ana ndoto za kwenda Ulaya kama mambo yatakaa vizuri.

SALEHJEMBE: Bado unaona unastahili kwenda kucheza Ulaya?
Sure Boy: Kabisa, kweli nina ndoto ya kucheza Ulaya kwa kuwa nina uwezo. Pia sina hofu ya umbo kama ambavyo wengi wamekuwa wakihofia.

SALEHJEMBE: Lakini umbo pia ni kigezo katika soka Ulaya, huoni umbo lako litakuangusha?
Sure Boy: Watu wanasahau tu, angalia Kante wa Leicester. Hana umbo kubwa lakini anafanya kweli na timu yake ipo kileleni. Kwani kuna viungo wangapi wana maumbo makubwa na hawajafanya vema? Mimi nitakomaa ikitokea na nchi yoyote ile.


SALEHJEMBE: Unafikiri viporo vinaweza kuisaidia Azam FC kuifikia Simba na mwisho kuipita?
Sure Boy: Hakika inawezekana. Tulikuwa na majukumu ya kimataifa, tunamalizia Jumapili halafu tunaendelea tena na ligi. Nia ya wachezaji, makocha wa Azam FC ni ubingwa. Sidhani kama itashindikana, maana tuna kikosi bora, pia tuna nia.

SALEHJEMBE:Unahusishwa na Yanga, kwamba mechi dhidi ya Yanga huwa unacheza kinazi, vipi unajali ushabiki badala ya kazi?
Sure Boy: Hakika hilo suala linaniumiza sana. Najisikia vibaya sana ikitokea kwa kuwa mimi ni kati ya wachezaji walioipandisha Azam FC. Najua uchungu wa timu hii.

SALEHJEMBE: Bado hujanieleza kuhusiana na unazi na kuacha kazi!
Sure Boy: Labda hujanielewa, mimi nina mapenzi makubwa na Azam FC. Sipendi watu wanichanganye na Yanga kwa kuwa timu yangu ni Azam na kazini kwangu ni Azam. Wanielewe na nisihusishwe na Yanga au Simba.

SALEHJEMBE: Umekosa kama mechi mbili au tatu za Yanga. Taarifa zinasema umekuwa ukiwekwa kando sababu wanahisi ni Yanga, hilo vipi?
Sure Boy: Kweli imetokea katika siku za hivi karibuni. Lakini ngoja na mimi nikuhoji. Nikiwa na Azam nimecheza mechi nyingi tu dhidi ya Yanga, zipo ambazo tumeshinda, sare au tukafungwa. Pia kuna zile ambazo nilitoa pasi za mabao dhidi ya Yanga pia Yanga inashiriki ligi lakini nimepambana na Azam tukatwaa ubingwa. Sasa huo Uyanga wangu umekuja siku hizi tu?

SALEHJEMBE:Huenda umewaonyesha siku hizi waziwazi?
Sure Boy: Hakika hakuna anayesema mimi nimeonyesha unazi vipi. Inawezekana kuna watu tu wanapeleka maneno kwa kocha au uongozi. Ushauri wangu waniache nicheze soka, niitumikie timu yangu. Nimeipigania sana Azam, ningekuwa siipendi ningehamia Yanga nikaiacha isipande daraja.


SALEHJEMBE:Kweli Yanga waliwahi kutaka kukusajili, ukakataa?
Sure Boy: Hilo pia ni suala lililotokea. Yanga walinipa Sh milioni 60 nisaini, mimi nikakataa. Azam wakanipa nusu yake nikasaini.

SALEHJEMBE: Kwa nini usikae na kocha na kumueleza kuhusiana na hilo?
Sure Boy: Kocha yuko poa kabisa, nimezungumza naye. Pia amekuwa na hofu naweza kukosea ikaonekana ni sababu ninaipenda Yanga, ananiweka nje lakini nimemuomba aniamini, mimi ni Azam FC. Mimi si Yanga wala Simba na hii ni kazi yangu.

SALEHJEMBE: Ikitokea Yanga wanakutaka itakuwaje?
Sure Boy: Soka ni kazi yangu, kama kuna makubaliano kupitia Azam, nitafanya kazi ila kwa sasa, akili na nguvu zangu ziko Azam.

SALEHJEMBE: Ukipewa nafasi utaonyesha kweli wewe si mnazi wa Jangwani?
Sure Boy: Mimi si mnazi na nafasi ya kucheza niliishapata. Tafadhali wanirudishe nifanye kazi yangu. Wauthamini mchango wangu, waone hili linaniumiza sana, naumia na kukosa raha.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic