July 8, 2016





Na Saleh Ally
KWA kipindi hiki hakuna mtu ambaye anaweza kuinua mkono na kusema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linafanya vizuri sana katika harakati zake za kuendeleza soka nchini.

Ukiona mtu anafanya hivyo, basi jua huyo ni shabiki au anataka kuwafurahisha baadhi ya viongozi wa shirikisho hilo kwa kuwa ni maswahiba wake au naye anafaidika na kuwepo kwao pale.

TFF imeboronga hadi imekuwa kero, imekosea mambo mengi sana kwa kuwa mwanzo wa hesabu zake ulikuwa ni ule wa kukurupuka. Katika viongozi wa shirikisho hilo, hakuna aliyewaza mipango endelevu, badala yake kila mmoja alifanya mambo kwa “mpango wa siku”.

Siku inapokwisha basi kila kitu kimeisha. Huu ndiyo umekuwa ni mwendo wa TFF na kitu kibaya zaidi ni hiki; hawataki kuambiwa kwa kuwa wanaamini kuelezwa ni kuhujumiwa.

Hakuna anayeihujumu TFF, zaidi inajimaliza yenyewe kwa ajili ya matatizo rundo kama kujaza watu wenye uwezo mdogo kwenye nyanja muhimu kwa kuwa tu ni maswahiba wa viongozi wa juu.

Tumeona inaandamwa na matatizo na kashfa kibao, sasa ni nguvu kubwa inatumika kuzifukia au kuzifunika zisiendelee kusikika wakati zinasikika kila kukicha.

Tunajua kuhusu uendeshaji wa ligi ulivyo na mapungufu, uwezo mdogo wa waamuzi, ratiba yenye viraka kupindukia. 

Imefikia hata asiyejua mpira anajua kipindi cha TFF chini ya Leodeger Tenga ambacho kimepita ni bora kuliko hiki cha Jamal Malinzi sasa.

Wadau wa soka, hata wale waliokuwa wakiutetea uongozi wa sasa au wengi wao, hawatamani tena na wao ‘wameanza’ kuamini kuwa kweli TFF inaboronga na inaonekana kushindwa.

Lakini leo, nina kitu nakubali kuwa tofauti kwamba pamoja na kuinyonga TFF, kuna jambo tunaweza kuipa kama haki, nalo ni mwendo wa Serengeti Boys ambayo wamemrudisha Kim Poulsen na hii ni baada ya kukubali kosa kwamba kuna mtu anayejiita mshauri, alishauri afukuzwe. Wakamlipa mamilioni na sasa wamemrudisha.

Poulsen raia wa Denmark anaongoza jahazi la Serengeti Boys akisaidiwa na Bakari Shime ambaye ni kocha mkuu. Timu inafanya vizuri katika michuano ya kimataifa na sasa inaonyesha dira, kweli inaweza kuwa mkombozi wa soka nchini na kuiondoa Taifa Stars hii ya machungu kila mwaka kwa Watanzania.

TFF inajitahidi kuonyesha iko tayari kukuza na kuendeleza vijana. Kwa kuwa imeshindwa kuzisimamia klabu kuwa na timu za vijana, angalau inaonyesha imepania kuona Serengeti Boys wanafanya vizuri zaidi.

Hadi sasa, TFF wanastahili pongezi kwa wanavyowalea vijana hao, wanavyoisimamia kambi yao. Ninaamini fedha kutoka Fifa kwa ajili ya maendeleo ya soka la vijana zitakuwa zinatumika vizuri ingawa imekuwa wakijisifia kwamba haina mdhamini na wao wanajitutumua!

Kwanza kukubali kuigharamia, ni jambo la kupongezwa. Mwendelezo tangu imeanza hadi sasa, hakika ni jambo jingine la kupongezwa kama watu wanaojali kabisa.

Ambacho ninaweza kukumbusha baada ya pongezi hizo, ni TFF kuweka utaratibu utakaowawezesha vijana hao kuendelea kuwepo. Utakaowafanya wajiendeleze zaidi kama kupata klabu au vinginevyo.

Kuwa na utaratibu wa kuwafuatilia badala ya kuwa kama vile enzi zile, baada ya vijana kumaliza mashindano mfano yale ya Afrika Kusini au Brazil, basi haijulikani wanafanya nini kipindi hiki maana wengi hawako katika mpira.

TFF si klabu lakini bado ina nafasi kubwa ya kuwashikilia vijana walioonyesha vipaji vya juu na kuhakikisha wanakua kisoka kwa mpangilio sahihi na baadaye kuja kuwa faida kwa taifa.

Tuliona Thomas Ulimwengu akikulia katika kituo cha kulea vijana chini ya TFF, leo ni tegemeo la Tanzania na gumzo la Afrika. Inawezekana kama wakiamua.









0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic