VIJANA WA KITANZANIA WAKIFURAHIA KOMBE NA MEDALI WALIZOSHINDA KATIKA MICHUANO ILIYOMALIZIKA PUNDE KATIKA MJI WA FREIBURG NCHINI UJERUMANI.. |
*Lakini
wamewaonyesha kuna matatizo pia ya kuyafanyia kazi
Na Saleh
Ally, Freiburg
Vijana wa
Kitanzania wamehitimu mafunzo yao ya miezi mitatu katika mji wa Freiburg hapa
Ujerumani na kuweka wazi mambo mengi sana ambayo yanaweza kutoa msaada katika
maendeleo ya soka nchini Tanzania.
Freiburg ni
mji ulio Kusini mwa Ujerumani ukiwa unapakana na nchi za Uswiss na Ufaransa,
karibu kabisa na mji wa Strasbourg aliozaliwa Kocha Mkuu wa Arsenal, Arsene
Wenger.
JAPHETERRY MAKARANGA AKIMTHIBITI KIUNGO WA FLUMINENSE YA BRAZIL |
Vijana hawa
walikuwa wameweka kambi yao nje kidogo ya Freiburg katika mji wa Hausen ambao
ni sawa na kijijini lakini maendeleo yake kwa nyumbani Tanzania, yako juu sana.
Walikuwa wakisoma pamoja na kufanya mafunzo mbalimbali ya mchezo wa soka.
Vijana hao
walikuwa 11, lakini hadi mwisho wanamaliza walikuwa wamebaki watano baada ya
Emily Mugeta kurejea Tanzania, mwezi mmoja kabla ya kwisha kwa mafunzo na
kujiunga na Simba ambayo alikuwa akiichezea.
FRANK SEKULE AKIAMBAA NA GOZI KATIKA MECHI DHIDI YA FLUMINENSE YA BRAZIL |
Wengine
waliomaliza mafunzo hayo walikuwa ni Frank Sekule, Japhet Vedastus, Miraji
Madenge, Kalos Kirenge na Rajabu Rashid.
Walikuwa
wakifanya mafunzo chini ya Fels Project ambayo ilikuwa inahusisha masuala ya
elimu ya maisha pamoja na soka. Lakini walikuwa wakifundishwa mambo lugha ya
Kingereza kwa ajili ya kuwasaidia katika mawasiliano.
WAKIWA NA FURAHA BAADA YA KWISHA KWA MASHINDANO |
Championi
liliripoti wakati wakiendelea na kozi kuanzia mwanzo na mafunzo hayo ya vijana
yanaonyesha kuna mambo mengi yanawezekana Tanzania, lakini mkazo na umakini
huenda umekuwa tatizo kubwa.
Mazingira:
Imeonyesha
wazi mazingira waliyokulia vijana hao, wengi wakiwa wanatokea katika kituo cha
TSC cha Mwanza ni magumu. Hivyo kunakuwa kuna ugumu wa juu katika masuala ya
elimu na uelewa katika maisha hasa katika dunia ya sasa.
Lakini
hakuna msaada wa kutosha, inawezekana kutoka kwa wazazi au jamii inayowazunguka
ambayo inataka iendeshe mambo kibabe na zaidi kuangalia ukubwa kwa kigezo cha
heshima.
Kwamba
malezi ya watoto wengi wa Kitanzania, hayatoi nafasi kwa watoto kujieleza au
kuchagua wanataka nini na badala yake ni uamuzi wa wazazi pekee na mtoto
anachotakiwa ni kutekeleza, hiyo inaitwa ni heshima lakini katika hali halisi
ni amri tu bila kuhoji.
Mafunzo:
Vijana
wengi wa KItanznaia bila ya kujali wanafikia wapi kisoka, wamekuwa wakijiinua
wenyewe kwa kiasi kikubwa bila ya msaada wa mafunzo.
Maana yake,
timu mwisho zimekuwa zikiangalia vijana wenye vipaji lakini bila ya kujali
kwamba wanastahili mafunzo na kuwafundisha mfano kuwa na shule bora za soka.
Badala
yake, wao wenyewe wanajitegemea na mwisho wanapata timu bila ya mafunzo na hali
hiyo imekuwa ikisababisha ugumu sana hasa kwa makocha wageni wanaotokea barani
Ulaya ambao hujaribu kufundisha kwa kufuata mfumo wa kisasa na kunakuwa na
ugumu.
Kwani
mafunzo anayoyapata mchezaji akiwa Yanga, Simba au Azam FC yanakuwa magumu kwa
kuwa anaanza mafunzo ya chuo kikuu bila ya kupitia yale ya shule ya msingi wala
sekondari.
Kujituma:
Bado
inaonekana kuna tatizo la kujituma kwa wachezaji wengi wa Kitanzania, huenda
pia wangejifunza hayo wakiwa katika shule za awali za soka ambazo wengi
hawapati nafasi ya kupitia huko.
Hivyo
inafanya vijana wengi wakwame katikati na wakati mwingine inakuwa ni lahisi
kuridhika na walichonacho au wanachokipata katika wakati husika.
Inaonekana
somo la kwamba maisha au kutimiza ndoto ya unachokitaka lazima ujitume halijawaingia
vizuri. Wangeweza kulipata tokea wakiwa makinda kwa kukumbushwa kila mara kwa
msisitizo, basi isingekuwa shida kwao ukubwani.
Hata hivyo
vijana hao waliokuwa hapa wameonyesha uwezo mkubwa kisoka, walikuwa wakijituma
na wahusika wa Fels Project wanaamini kutokana na mazingira waliyopitia basi
wamejitajhidi sana kwa kiasi sana.
Pamoja na
mambo mengine, lakini walifanikiwa kupata vikombe na medali na zaidi
vilihusiana na suala la Fairplay, kitu ambacho ni bora pia kwa maana ya
kutambua mchezo wa soka unataka nini.
Kutokana na
mazingira waliyokulia hadi kufikisha kuanzia miaka 18, vijana hao wameweza
kuishi katika mazingira ya Ujerumani na kufanya vizuri kabisa.
Hii ni
dalili kwamba kila jambo linawezekana lakini msingi mzuri ndiyo uti wa mgongo,
pia ni vema kukawa na hali ya kuonyesha kweli vijana wanapaswa kuandaliwa tokea
wakiwa wadogo.
0 COMMENTS:
Post a Comment