Na Saleh
Ally
KUNA watu
ambao hupaswa kupewa heshima yao, lakini inawezekana kabisa wakawa hawaipati
kwa kuwa wanaotakiwa kufanya hivyo wanakuwa hawafikirii mambo mengi kuhusu wao.
Mshambuliaji
wa Azam FC, Gaudence Mwaikimba ni kati ya wachezaji wanaopaswa kupewa heshima
ya kuwa mmoja wa wachezaji wanaoendelea kung’ara katika Ligi Kuu Bara pamoja na
kuhama timu moja kwenda nyingine.
Mwaikimba, msimu
huu amefikisha zaidi ya misimu saba akiwa kwenye ligi hiyo, lakini bado
ameendelea kuwa nyota na mchezaji muhimu kwa kila njia.
Azam FC
imetwaa ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Mbeya City
siku chache tu zilizopita, lakini Mwaikimba ambaye amekuwa chachu na mhimili wa
mechi za mwisho za timu hiyo, yeye amefikisha kombe la nne.
Mwaikimba
ametwaa makombe matatu ya Ligi Kuu Bara akiwa na Yanga, sasa ameongeza moja
akiwa na Azam FC, maana yake ni kati ya wachezaji wachache wanaocheza ligi kuu
wakiwa na mataji kama yake.
Hiyo ni
sehemu ya kuonyesha mshambuliaji huyo ambaye hana makeke na aliyekuwa kipenzi
cha mashabiki wa Yanga wakati anaichezea timu hiyo, anastahili heshima yake
kutokana na kazi yake nzuri kwa kipindi kirefu sasa.
Kocha Joseph
Marius Omog raia wa Cameroon alisema Mwaikimba atapewa nafasi katika mechi za
mwisho kwa kuwa ana kazi maalum ya kufanya. Kweli mechi mbili za mwisho ambazo
Azam ilijihakikishia kutwaa ubingwa baada ya kuwa inahitaji pointi sita tu,
Mwaikimba akafanya kazi yake.
Mechi dhidi
ya Ruvu Shooting ambayo siku ya kwanza iliahirishwa kutokana na mvua kubwa,
ilipopigwa siku iliyofuata, Azam FC ikashinda kwa mabao 3-0 na Mwaikimba
alikuwa wa kwanza kufungua mlango wa wanajeshi hao ambao walikuwa hawajafungwa
kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Mabatini, Mlandizi.
Azam FC
ikawa imebakiza pointi tatu tu kuwa bingwa na kazi ilikuwa ngumu maana ni dhidi
ya Mbeya City, Mwaikimba akaanza tena, safari hii akiwa na John Bocco na bila
ajizi, Mwaikimba akafunga bao la kwanza wakati timu yake ikishinda mabao 2-1 na
kutwaa ubingwa Bara.
Mwaikimba
amecheza Ligi Kuu Bara tangu akiwa na Tukuyu Stars ya Mbeya, baadaye Ashanti
United, Yanga, Kagera Sugar na Moro United kabla ya kutua Azam FC.
Hakuna
anayeweza kukataa suala la Mwaikimba kupewa heshima yake kwa mengi, kuwa mmoja
wa wachezaji wachache wenye mafanikio. Amecheza timu kubwa, ndogo lakini
ameendelea kukusanya mafanikio.
Mwaikimba
ameliambia Championi Jumatano kwamba, mara kadhaa watu wamekuwa wakisema
amekwisha, lakini hawafanyi tathmini vizuri.
Kuisha:
Watu
hawafanyi tathmini, hauwezi kusema mtu ameisha wakati hachezi. Inawezekana
mfumo tu wa kocha, ndiyo maana unaona nikicheza ninafanya vizuri. Watu wapime
mtu anayecheza na asiyecheza.
Kukata
tamaa:
Usipokuwa
makini unaweza kukata tamaa, lakini kwangu ni tofauti kwa kuwa ninajiamini lakini
nina moyo wa subira, pia ninaamini kwenye nafasi kwamba siku ikifika nitapata
na mimi nitacheza. Lakini kawaida, ninamuunga mkono anayecheza namba moja na
mimi.
Mfano John
(Bocco), anapocheza ninamuunga mkono kwa kuwa pointi tatu kwa timu ni kwa wote.
Siku na mimi nikipata nafasi, najitahidi kufanya vizuri. Angalia mechi dhidi ya
Ashanti United, Bocco na Kipre (Tchetche) hawakucheza, tulishinda bao nne na
nikafunga mawili.
Mechi:
Sijacheza
mechi nyingi, nyingi niliingia lakini nimeanza mechi sita na nimefunga mabao
matano. Ninauamini uwezo wangu, ninalalia kwenye subira ndiyo maana utaona
ninaendelea kufanya vizuri.
Azam FC
sasa timu kubwa, hilo watu lazima wakubali. Kama ningekuwa sina uwezo,
wasingenibakiza hapa, wanajua nina uwezo upi na mimi nasisitiza najiamini.
Kocha:
Kweli
alisema kuna mechi ningecheza, kanipa nafasi sikumuangusha kocha (Omog). Kwangu
hata kama sikucheza mechi nyingi namuona ni kocha bora na alibadili sana
uchezaji wetu.
Utaona
uchezaji wa Azam FC ugenini na nyumbani ulikuwa tofauti, kulikuwa na maelekezo
yake. Hivyo ni kocha anayejua nini anachofanya hadi sasa.
SOURCE: CHAMPIONI JUMATATU
0 COMMENTS:
Post a Comment