Kocha Mkuu wa Simba, Mcroatia, Zdravko Logarusic, amekataa usajili
wa kiungo mkabaji, Antony Teddy na mshambuliaji Rama Salim wanaoichezea Klabu ya
Gor Mahia ya Kenya.
Mwingine aliyetemwa ni Dan Sserunkuma ambaye ni raia wa Uganda,
lakini anakipinga kwenye kikosi cha Gor Mahia.
Awali zilikuwepo tetesi za timu hiyo iliyomaliza Ligi Kuu Bara
ikiwa kwenye nafasi ya nne kuwasajili wachezaji hao kwa ajili ya kukiimarisha
kikosi chao katika kuelekea msimu ujao.
Timu hiyo katika msimu uliopita ilishindwa kufanya vizuri kutokana
na kikosi chao kutoimarika kwenye baadhi za nafasi ambazo Mcroatia huyo
amewasilisha ripoti ya usajili kwenye kamati ya utendaji ya timu hiyo.
Akizungumza karibu na mji wa Zagreb, Croatia,
Logarusic alisema katika ripoti yake aliyoikabidhi kwenye kamati ya utendaji,
hahitaji mchezaji yeyote wa kutoka nje ya nchi.
Logarusic alisema katika ripoti yake, ametoa mapendekezo ya usajili
wa wachezaji wazalendo na siyo wa kigeni kutokana na timu yao kutoshiriki
michuano ya kimataifa mwakani.
“Katika ripoti yangu ya usajili niliyoikabidhi kamati ya utendaji,
hakuna sehemu yoyote iliyotaja nahitaji mchezaji kutoka nje ya nchi, badala
yake nataka wazawa na hizo taarifa nyingine zinazosemwa ni tetesi.
“Nimetoa mapendekezo ya usajili ya baadhi ya wachezaji wazawa
niliowaona msimu uliopita ambao kama wakiwasajili basi timu yetu itachukua
ubingwa,” alisema Logarusic na kuongeza:
“Hivi karibuni nilizungumza na mmoja wa watu wa karibu wa Simba
akinitaka niangalie wachezaji wanaofaa kutoka Kenya kwa ajili ya kuwasajili,
lakini nilizuia usajili wa maprofesheno na kumtaka tusajili wazawa pekee,”
alisema Logarusic.
0 COMMENTS:
Post a Comment