UKIANGALIA
mambo yanavyokwenda katika klabu ya Simba katika kipindi hiki, hayaridhishi, si
ya kiuanamichezo na inaonekana wazi kuwa kuna makundi na sasa hakuna anayewaza
maendeleo ya klabu au kikosi cha Simba.
Hakuna
anayeweza kukataa kuwa Simba wanavurugana katika kipindi hiki na tafrani zote
zinatokana na makundi yanayotokana na uchaguzi, wengine wanamtaka huyu, wengine
yule.
Kama kuna
mtu atakuwa anafurahia kinachotokea Simba kwa watu kugombea fito, atakuwa ni wa
ajabu sana. Angalia maneno ya kashfa, kudhalilishana hadharani na wengi
wakionekana kutojali lolote, si sahihi!
Sasa ajabu,
inaonekana hata baadhi ya wanachama wa Yanga wanaonekana kuvutiwa na hilo,
huenda wanatamani kinachotokea Simba basi kianze Jangwani. Wanasema wanapinga uamuzi
wa wanachama wenzao zaidi ya 4,000 kumuongezea mwaka mmoja madarakani
Mwenyekiti wao na uongozi wake.
Yusuf Manji
aliongezewa mwaka mmoja na wanachama hao kwenye mkutano uliofanyika wiki
iliyopita jijini Dar es Salaam. Kweli, ajenda haikuwa hiyo, badala yake ni
kupitia marekebisho ya katiba kutokana na maagizo ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF).
Manji
hakuanzisha ajenda hiyo, badala yake wanachama pamoja na wajumbe wa baraza la
wadhamini ambalo Mwenyekiti wake ni Mama Fatma Karume ambaye hauwezi ukasingizia
eti ana njaa ndiyo maana alifanya vile kwa kuwa amehongwa au kupata mlungura.
Kumbuka Mama
Karume ni Mama wa Taifa, marehemu mumewe, Abeid Aman Karume ni kati ya
waliopigania maendeleo ya Yanga kwa kiasi kikubwa wakati wa uhai wake. Ulizia
ndiye chanzo cha jengo la makao makuu ya klabu hiyo. Sasa vipi mkewe afanye
kitu ambacho si sahihi na kitaiangamiza klabu hiyo.
Manji
alipewa miaka nane na wanachama hao, lakini yeye akaona sahihi au angalau
mmoja, sasa vipi anapaswa kupopolewa. Vipi anayekataa alishindwa kwenda kwenye
mkutano.
Hakuwepo,
anaweza kupinga kilichoamuliwa na wanachama karibu wote hai wa Yanga? Kama
kweli ni demokrasia, vipi wanaopinga wasifuate utaratibu badala ya kuzungumza
maneno mengi ya kashfa kuhusu Manji?
Inawezekana
kabisa kuna makosa kafanya, lakini mangapi na pia wasisahau ni mazuri mangapi
kafanya kwa ajili ya Yanga. Pia kuna sababu ya kukumbuka, kwa wanaomlaumu Manji
wameifanyia nini Yanga au ndiyo kupiga mdomo tu!
Kingine
kizuri kinachotakiwa ni wanaochambua hoja ya Manji na uongozi wake kuongezwa
mwaka mmoja iwe hivi, wapitie vipengele vya katiba na kueleza kwamba wamekiuka
katiba au ni sahihi. Si sahihi kulalama tu kama hewa!
Yanga
wanapaswa kuepuka vitu ambavyo vinaweza kusababisha wao kuingia kwenye
malumbano, chuki kama ambavyo hali imefikia sasa Simba. Watu wanaishi kwa
kuwindana, kila mmoja anaangalia wapi pa kumtukana au kumdhalilisha mwenzake.
Waliompinga
Manji, mwanzo kabisa wameanza na maneno ya kashfa ambayo mwenyekiti huyo
hastahili. Lakini kama wanataka kumkosoa, ziko njia sahihi na vema watumie hoja
za msingi.
Soka ni
fedha, soka linahitaji wapanga mipango na wanaotaka kuutumikia mchezo huo kwa
dhati. Hakuna haja ya kuona haya, Yanga na mchezo wa soka nchini unahitaji watu
kama Manji, wenye nguvu kifedha, uwezo wa kupanga na kutekeleza na si wale
wanaotaka kuingia madarakani ili wafaidike.
Sasa vipi
kila mwenye uwezo analazimishwa kuwa adui, kwa kuwa tu kuna watu hawamkubali
kwa kuwa alikataa kuwasaidia kwenye kampeni zao za kisiasa au mambo yao ya
kimaisha. Sasa hayo ndiyo maslahi ya Yanga au soka ya Tanzania.
Vizuri
Wanayanga wajiulize mara nyingi, huu si muda wa kuzozana na wapenda soka
wasingependa malumbano kama yale ya Simba. Watu wanahitaji mipango na soka la
uwanjani, si maneno mengi na
blahbla tu!
0 COMMENTS:
Post a Comment