October 1, 2014


Na Saleh Ally
MECHI mbili za Ligi Kuu Bara kwa kila timu zimewaacha baadhi ya wachezaji na makocha wakiwa na kazi kubwa ya kubadili mambo kutokana na walichokifanya.

Wanalazimika kuyabadili mambo kutoka kwenye ‘no’ kwenda kwenye ‘yes’, la sivyo watapoteza umaarufu au imani yao kwa mashabiki wa timu zao. Wapo wengi lakini hawa wachache, kazi wanayo.

Phiri:
Hakuna asiyejua uwezo wa juu wa kazi ya Patrick Phiri, lakini katika mechi mbili, Simba imepata pointi mbili. Safu ya ulinzi imefungwa tatu, washambuliaji wamefunga tatu!
Ni kiwango cha kawaida sana na mechi dhidi ya Stand United, lazima abadili mambo la sivyo, hofu itaanza kuwatafuna Wanasimba na mwisho watageuza ubao kwa Mzambia huyo.

Maximo:
Timu yake imecheza mechi mbili, ina pointi tatu baada ya kuifunga Prisons ya Mbeya kwa mabao 2-1, lakini kwa tabu kwelikweli. Uwezo wa kazi yake unajulikana, lakini hawezi kukwepa kwamba kazi ya ziada inatakiwa.
Yanga ilicheza vizuri mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, ikafungwa mabao 2-0, ilipocheza hovyo ikashinda. Hivyo bado imekaa vibaya kwake.
 
JAJA
Jaja:
Tayari ameichezea Yanga mechi mbili lakini hajafunga hata bao moja, ana kazi ya kubadilisha wanachoamini mashabiki wa Yanga na wengine, kwamba si mkali kihivyo.
Anajulikana ana uwezo wa kufunga mabao, lakini bado haitoshi mambo kubaki kwenye hadithi tu, badala yake lazima aanze kuonyesha na hasa katika mechi mbili zinazofuatia dhidi ya JKT Ruvu na Simba.

Olaba:
Tom Olaba ni kati ya makocha bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki na amethibitisha hilo akifundisha kwao Kenya na hapa Tanzania.
Msimu huu kaanza kwa vipigo viwili, watu hawataki ubora kwenye historia badala yake kilichopo. Lazima akichangamshe kikosi chake cha Ruvu Shooting, la sivyo atakutana na kibuti.
 
MAGULI
Maguli:
Ingawa Elias Maguli amekuwa akiingia dakika za mwisho, lakini hajaonyesha kuwa ni hatari au ana msaada mkubwa Simba. Analazimika kubadilika na kuthibitisha kuwa Simba walipatia kupambana kumpata kwa kuwa ana msaada wake. Mechi mbili zijazo, atalazimika kuwa na majibu.

Kiiza:
Msimu uliopita Mganda Hamisi Kiiza alidoda hasa wakati ligi ikienda ukingoni. Lakini msimu huu ni zaidi ya kudoda kwa kuwa hajaonyesha lolote. Nafasi aliyopewa si kubwa, lakini inavyoonekana amezidi kuporomoka. Akiendelea hivyo, hakuna ubishi atauona mlango wa kutokea kwenye dirisha dogo.

MWAMBUSI

Mwambusi:
Matumaini ya mashabiki wa Mbeya City yako juu sana kutokana na rekodi nzuri ya msimu uliopita, kupanda na kushika nafasi ya tatu. Kocha Juma Mwambusi lazima apambane kuhakikisha mambo yanabadilika maana alianza na sare dhidi ya JKT akiwa nyumbani na kupata ushindi wa shida, huku wageni Coastal Union wakilalamikia penalti, hii inaonyesha analazimika kubadili mbinu.

Kiongera:
Paul Kiongera kweli ameumia, lakini mechi mbili alizoichezea Simba hakuwa na msaada wowote. Lazima aamini anajiuguza lakini ana deni kubwa kwamba lazima aonyeshe sababu ya yeye kukabidhiwa jukumu la kufunga mabao.

Minziro:
Fred Felix Minziro, ndiye kocha wa JKT Ruvu na kikosi chake hakina mwendo mzuri. Mechi mbili kina pointi moja. Mechi inayofuata ni dhidi ya Yanga wenye hamu ya kutaka kushinda, ana kazi ya kuonyesha ubora wa kazi yake.

Isihaka:
Beki Hassan Isihaka ni kinda, kuondoka kwa Donald Musoti kumempa nafasi ya kucheza. Lakini ameshindwa kuonyesha uwezo, ameingia kwenye makosa yaliyochangia Simba kudorora. Akipewa nafasi tena, lazima abadilike, la sivyo ‘atafia’ benchi.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic