Wakati Simba wakiwa tayari wameanza mazoezi
ya nguvu, kwa ajili ya mtanange mkali wa Nani Mtani Jembe 2 dhidi ya Yanga,
kocha mkuu wa klabu hiyo, Mzambia, Patrick Phiri, anatarajia kutua nchini kesho
Alhamisi.
Phiri, ambaye aliondoka nchini wiki
iliyopita, anatarajiwa kurejea nchini kesho kwa ajili ya kuendelea kuiandaa
timu hiyo.
Hata hivyo, wakati Phiri akitarajiwa
kutua nchini kesho, Kocha wa Yanga, Marcio Maximo atashuka Bongo leo, akitokea
kwao Brazili sambamba na kiungo mpya Emerson Roque ambaye atakuja kwa ajili ya
majaribio.
Akizungumza na Championi Jumatano
jana, Katibu Mkuu wa Simba, Stephene Ally, alisema kuwa Phiri anatarajia kutua
nchini kesho, tayari kwa ajili ya kukiandaa kikosi chake kujiweka fiti kuelekea
mchezo wa kukata na shoka dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga utakaopigwa
Desemba 13, mwaka huu.
“Kama hakutakuwa na matatizo yoyote,
basi kocha atatua nchini keshokutwa (Alhamisi) kwa ajili ya kuendelea na
majukumu yake, ikizingatiwa tuna mchezo mkubwa mbele yetu, hivyo anatakiwa
kurejea mapema,” alisema Ally.
Ikumbukwe Simba ndiyo wanashikilia
ubingwa huo ambao waliutwaa msimu uliopita kwa kuilaza Yanga mabao 3-1.
0 COMMENTS:
Post a Comment