KIFARU. |
JINA la Thobias Kifaru siyo geni katika soka la
Tanzania, huyu ni Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar akidai kuwa amedumu katika cheo
hicho kwa miaka 25 klabuni hapo.
Kifaru ambaye aliwahi anasema aliwahi kuichezea timu
hiyo mwaka 1983 akiwa kipa ambapo kipindi hicho ilikuwa timu ya kujifurahisha
kutoka Kiwanda cha Mtibwa Sugar, ni mmoja ya waanzilishi wa timu hiyo ambayo
ilianza rasmi yapata mwaka 1983 ikiwa chini ya kaka yake aliyefahamika kwa jina
la John Kifaru.
“Mwanzoni tulikuwa tunacheza kujifurahisha, baadaye
tukaingia katika ushindani mwaka 1984 kwa kuanzia Ligi Daraja la Nne ambapo
mimi nilikuwa kipa lakini tulipofika la tatu sikuendelea kucheza, iliendelea
hivyo mpaka mwaka 1996 ilipofika Ligi Kuu Bara enzi hizo ikitambulika kuwa Ligi
Daraja la Kwanza.
“Niliacha kucheza nikaendelea na majukumu yangu ya
kuajiriwa pale kiwandani kwa sababu mimi ni mtu IT (Information Technology)
lakini huku naendelea kusimamia timu hapo mwanzilishi wa timu kaka yangu
alikuwa amefariki mwaka 1993 na mlezi wa timu alikuwa ni Sosteness Magese baba
mzazi wa Happiness Magesse huku nikiendelea na kazi hiyo pamoja na uandishi wa
habari wa kujitegemea.
Ilikuwaje ukawa msemaji?
Mwaka 1996 kama sijakosea nikiwa nafanya kazi ya
uandishi pale katika Gazeti la Nipashe na vyombo vingine vya habari, Maulid
Kitenge akiwa anasoma ndiyo alianza kuniita msemaji, tangu hapo mpaka leo
nikawa msemaji wa Mtibwa Sugar.
Timu yako ikifungwa hali inakuaje?
Naumia lakini siyo kuwa nashindwa kuzungumza, mimi kabla
na baada ya mechi naongea bila kujali aina ya matokeo.
Kipi hutasahau katika kazi yako?
Miaka mitano iliyopita niliacha kufanya kazi kwa
takribani mwaka baada ya kuhusishwa kuwa nilichukua rushwa kwa Azam FC baada ya
kutufunga mabao 3-0.
Kilichonifanya nihusishwe ni kitendo cha kuwakaribisha
kule Manungu na kuwaonyesha hoteli ya kufikia na njia za kupita. Mwenyekiti
kipindi hicho alikuwa Ali Mhina alinituhumu kuchukua rushwa, niliumia sana.
Baada ya kuona klabu inapotea ilibidi mkurugenzi wetu,
Jamary Bayser awatumie viongozi kama wakina Bernard Kihaule na Salum Kijazi
kuniomba msamaha baada ya kugundua zilikuwa ni chuki binafsi, nilikubali
nikarudi kuendelea na kazi.
Kuhusu tambo kabla ya mechi
Nina uzoefu sana na klabu za Tanzania, nipo karibuni
miaka 25 kila timu naijua ndiyo maana huwa nazichambua vizuri na siyo kwamba
nakurupuka tu.
Siri ya Mtibwa kufanikiwa ni nini?
Tulijipanga mapema na kwa kuwa timu yetu inaongozwa
kikampuni ndiyo maana inakuwa rahisi kwa sababu kila kitu kinachohitajika kwa
wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi kinapatikana.
Kitu gani hupendi?
Sipendi kufananishwa na wasemaji wa klabu nyingine ambao
wamekuwa hawazitendei haki klabu zao kwa kutotoa ushirikiano mzuri kwa vyombo
vya habari.
Unapokea simu ngapi za ‘media’?
Siku za mechi ndiyo huwa napata shida sana lakini sina
jinsi ndiyo majukumu yangu, huwa naongea na simu zaidi ya 50 kutoka kwa
wanahabari.
Naweza kutumia saa tatu kujifungia ofisini, sirudi nyumbani
mpaka nitakapomaliza kazi yangu hiyo.
Hapo TFF ndiyo wanatakiwa kutufikiria kutupa fedha kwa
sababu wasemaji ndiyo tunaojaza watu uwanjani kwa mbwembwe zetu.
Simba, Yanga zimewahi kukufuata?
Ndiyo, Simba walimuagiza kiongozi wao wa hapa Morogoro
kuwa wananihitaji lakini sikuwa tayari kwa sababu naipenda klabu yangu.
0 COMMENTS:
Post a Comment