Na Saleh Ally
WAKATI fulani kulizuka mzozo mkubwa sana kati ya mmoja wa viongozi
wa wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali na mchambuzi wa michezo wa Clouds FC,
Shaffi Dauda na ishu kubwa ilikuwa Kocha Marcio Maximo.
Taarifa zilizagaa kwamba Dauda alimzuia Maximo kuja kuifundisha
Yanga wakati klabu hiyo ikifanya juhudi za kumnasa kutoka kwao Brazil.
Ilielezwa Dauda alimueleza akija Tanzania kuifundisha Yanga ataaibika bure.
Baadaye ilionekana Akilimali alikosa ukweli, mwisho akamuomba Dauda
aliyekuwa ametishia kwenda mahakamani yaishe. Naye akamsikiliza mzee wake na
kufunika kombe.
Baadaye Yanga ilimpata Ernie Brandts akaja kufanya kazi yake.
Alitimuliwa katika mechi iliyopita ya Nani Mtani Jembe, nafasi yake
ikachukuliwa na Hans van der Pluijm, akaondoka halafu akaja Maximo, naye
ametimuliwa kwenye Nani Mtani Jembe 2, mwaka huu.
Hesabu zinaonyesha tangu tafrani la Dauda na mzee Akilimali, hadi
Maximo anaajiriwa na kutimuliwa, haujavuka hata msimu mmoja! Kweli amevunjiwa
heshima yake.
Tuanze kwa kuangalia hesabu sahihi za mechi na michezo kama kweli
kocha huyo Mbrazili aliyewahi kuinoa Taifa Stars alistahili kufutwa kazi na
uongozi wa Yanga au ulifanya mambo yake kwa jazba tu!
Msimamo:
Wakati Maximo anatupiwa virago, tayari Ligi Kuu Bara ilikuwa
imechezwa kwa mechi saba kwa kila timu. Yanga ilikuwa katika nafasi ya pili
ikiwa na pointi 13, ambazo ni mbili pungufu dhidi ya vinara Mtibwa Sugar.
Ukirudi kwenye mabao ya kufunga, Yanga ina 9, inashika nafasi ya
pili baada ya vinara Mtibwa Sugar wenye 10.
Kwenye kufungwa, pia haikuwa na safu imara sana lakini si mbovu kwa
kuwa imefungwa mabao matano wakati vinara Mtibwa wamefungwa matatu tu na ndiyo
timu iliyofungwa mabao machache zaidi.
Maximo Vs Phiri, Omog:
Hadi anaondolewa, Maximo ndiye kocha wa kigeni aliyekuwa juu zaidi
kwenye msimamo kuliko makocha wengine wote.
Joseph Omog wa Azam FC, aliongoza kikosi chake katika mechi saba
akafanikiwa kufikisha pointi 13 kama za Maximo lakini akabaki katika nafasi ya
tatu kutokana na mabao ya kufunga na kufungwa.
Azam FC ilifunga mabao nane ikaruhusu manne, maana yake safu zote
mbili za ushambulizi na ulinzi zilikuwa dhaifu ukilinganisha na zile ya Yanga.
Yusuf Chippo raia wa Kenya, yeye aliiongoza Coastal Union kushika
nafasi ya nne, ikiwa na pointi 11. Ilifunga mabao 9 kama ya Maximo na kufungwa
saba.
Mganda, Jackson Mayanja wa Kagera Sugar alishika nafasi tano akiwa
na pointi 10, alifunga sita na kufungwa nne.
Patrick Phiri kutoka Zambia, aliiongoza Simba kuangukia nafasi ya
saba katika mechi saba ikiwa imefunga mabao saba na kufungwa sita.
Kocha mgeni ambaye kikosi chake kimefeli kabisa ni Tom Olaba raia wa
Kenya ambaye baada ya mechi saba, Ruvu Shooting ilishika nafasi ya 12, ikiwa na
pointi 6 tu, imefunga mabao 6 na kuchapwa 7.
Kwa maana ya hesabu au takwimu za michezo, hakika Maximo alitakiwa
kuwa kocha mgeni wa mwisho kutimuliwa nchini kama ungechukua wageni wote
wanaofanya kazi ya ukocha katika Ligi Kuu Bara.
Unaweza kusema angekuwa na nafasi ya kujirekebisha baada ya hapo na
hasa baada ya Yanga kufanya usajili kujiimarisha lakini safari imemkuta.
Rekodi:
Kwa upande wa rekodi nzuri na mbaya, huenda zimechangia kwa Maximo
kuondolewa nchini.
Maximo hashauriki, Maximo mbishi na anajua kuliko yeyote, huenda
akawa na ‘haki’ ya kumdharau kocha yeyote nchini kwa kuwa anatokea Brazil.
Imekuwa ni siri, lakini wasaidizi wake na wengi walio kwenye benchi
la ufundi hawakufurahia uongozi wake wa kibabe, hakupenda kushauriwa na kwa
kuwa ni kocha mkuu, basi alikuwa ni mwenye kauli ya mwisho.
Aliwahi kuonyesha tabia kama hizo vikiwemo visasi wakati akiwa Taifa
Stars. Watu wakamtetea lakini huenda wakati huu ulikuwa mzuri kuonyesha vizuri
upande wa pili wa shilingi ya Mbrazili huyo.
Hakuna anayefanikiwa bila ya kushirikiana na wenzake, hakuna
anayeweza kukibadilisha kitu kwa kuonyesha anajua peke yake. Ushirikiano ndiyo
namba moja.
Hakuna ubishi kwamba wako watu wenye vipaji katika soka, uandishi na
kazi nyingine lakini wanaweza kushindwa kufika mbali kutokana na tabia zao za
kibinadamu na hasa ujeuri au viburi.
Kwa tathmini hii, kwa hesabu zinaonyesha bado Maximo alipaswa kubaki
Yanga. Kitabia kuanzia kwenye enzi za Taifa Stars, acha tu Maximo aende kwao.
Tatizo lako Saleh usimba umekujaa sana hata kuona vilivyohai huwezi,wewe ongelea mambo ya Ndumbaro anayekuweka mjini ya Yanga waachie akina bin Zubeir!
ReplyDeleteSaleh yuko sahii sana tu
ReplyDeleteHata mimi ni shabiki wa Yanga, ila Salehe kiukweli ni mwandishi mzur. Nakuunga mkono Salehe ameongea ukweli kabisa.
Delete