Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe kusema kiungo Shabani Kisiga anajisumbua kwa kuondoka kambini, Kisiga mwenye ameibuka na kutoa mkono wa kwaheri.
Kiungo huyo alitimka kwenye kambi ya kikosi
hicho mara baada ya mchezo wao dhidi ya Mbeya City, ambao ulichezwa Jumatano
wiki iliyopita ambao timu hiyo ilifungwa mabao 2-1 na hadi sasa ameshindwa
kurejea huku uongozi ukijiumauma.
Awali, uongozi wa Simba ulisema kuwa mchezaji
huyo alikuwa na ruhusa maalum, lakini mwenyewe amefunguka kuwa hakuwa na ruhusa
na hawezi kurudi tena.
Kiungo huyo
alifunguka kuwa, mpira wa hapa Bongo umejaa siasa nyingi, hususan kwa klabu
kubwa kama ya Simba, viongozi wanashindwa kushikamana na kuweza kuitengeneza
timu na kuwa kitu kimoja.
Kisiga alisema kuwa viongozi wanatakiwa
kubadilika si kwa Simba pekee hata timu nyingine endapo tu wanaoutakia mema
mpira wetu na hii ndiyo inawafanya wachezaji kuwa na morali ya chini na
kushindwa kufanya vizuri.
“Nipo nyumbani kwa sasa na sipo kambini na
timu, nipo napumzisha akili yangu lakini Simba sirudi tena kuichezea, ingawa
nafahamu kuwa nina mkataba nao, jinsi hali ilivyo kwa sasa siwezi kurejea kule
na siwezi kucheza pale.
“Mimi najitambua, nafahamu kitu gani nafanya
kwa sababu nimekuwa katika soka kwa muda mrefu, lakini inaonekana siasa
zinaumaliza sana mpira wetu.
“Mpira siku zote ni ushindani na kama timu
kuanzia viongozi, wachezaji tunatakiwa kuwa kitu kimoja ili kuweza kuwa na
mafanikio, lakini Simba imekuwa tofauti kabisa katika suala hilo, kila mtu yuko
bize na lake, kweli hapo timu itaweza kufanya vyema kweli?
“Na lawama zimekuwa zikielekezwa kwa wachezaji
na makocha pekee, jambo ambalo siyo sahihi, kama klabu tukiwa pamoja na lengo
moja hakuna ambalo litashindikana na kuanza kutafuta mchawi nani, lazima
tubadilike katika hilo,” alisema Kisiga.
0 COMMENTS:
Post a Comment