Na Saleh Ally
NAANZA kwa
kukumbushia ule msemo wa ‘kisela’ kuwa hakuna mtu mwenye uwezo wa kuipiga
chenga njaa.
Wapenda michezo
wameuongezea utamu msemo huo kwa kusema hivi; “Hata uwe mshambuliaji mkali
vipi, hauwezi kuipuga chenga njaa.”
Lakini bado
kila mmoja mwenye kupenda mchezo wa soka, halafu akaweka kando ushabiki atakuwa
na nafasi ya kumpongeza mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi ambaye alifunga
bao la aina yake wakati timu yake ikiishinda Yanga kwa bao 1-0 katika mechi ya
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Mashabiki 49,758
waliolipa viingilio kushuhudia mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga kwenye
Uwanja wa Taifa, Jumapili, hakuna hata mmoja ambaye alijua alikuwa akifikiria
kwamba Mganda huyo angeweza kuupiga mpira huo na kumpita kipa Ally Mustapha ‘Barthez’
na kutinga wavuni.
Kweli Barthez
alifanya kosa, lakini huenda ukubwa wa kosa lake unaboreshwa na akili nyingi
alizozitumia Okwi katika kuupiga mpira huo akiwa katika kasi.
Takribani mita
35 tokea alipopiga na kufunga, kwa kipa yoyote si lahisi kutegemea mshambuliaji
anaweza kufanya hivyo tena akiwa karibu na beki.
Unakumbuka
mabao ya David Beckham au lile la Wayne Rooney, ni sehemu ya mabao ya aina hiyo
kufungwa uwanjani pia ni nadra kutokea.
Si vibaya
kusema tokea Uwanja wa Taifa uanze kutumika, lango ambalo amefunga Okwi,
halijawahi kufungwa kwa bao la aina ile. Angalau lango la Kaskazini, yaani
upande wa Simba, litakuwa na kumbukumbu ya bao safi la Jaja aliyekuwa akikipiga
Yanga wakati ikiadhibu Azam FC kwa mabao 2-0 katika mechi Kombe la Jamii.
Sasa kwa bao
kama lile la Okwi, utaona mechi inayofuatia Barthez anakaa nje, utaona
mashabiki wa Yanga wanalalamika, utaona taarifa zinasema kwa kuwa ametokea
Simba!
Barthez amedaka
zaidi ya mechi saba kwa ufasaha mkubwa na hata siku hiyo amefungwa bao moja,
bao bora na si zaidi! Bao ambalo kila aliyekuwa akiangalia mpira uwanjani au
mamilioni ya mashabiki waliokuwa wakishuhudia kupitia runinga, hakuna hata
mmoja alijua Okwi angefanya alichotekeleza.
Nilizungumza na
makocha wawili, Goran Kopunovic wa Simba na Hans van der Pluijm wa Simba, kila
mmoja alisema hakutegemea itakuwa vile.
Pluijm alisema
umakini wa mabeki kuhakikisha Okwi hafanyi uamuzi ulichangia yeye kupiga,
lakini akakiri kihesabu Barthez alikuwa amepotea.
Kocha wa Simba,
yeye alisisitiza mfumo wa kushambulia kwa haraka waliojifunza ulisaidia. Lakini
akaongeza kuwa Okwi anapaswa kupongezwa kwa kazi nzuri aliyoifanya na uamuzi wa
kishujaa kujaribu akiamini atafanikiwa.
Huenda bao hilo
la Okwi likazua kila aina ya tafrani na hasa upande wa Yanga, kitu ambacho
kinaweza kisiwe sahihi.
Kikubwa ni
kukubali kama ambavyo tulikubali ubora wa bao la Jaja. Kwamba kweli, Okwi
amefunga bao bora kabisa, bao linaweza kuwa funzo kwa washambuliaji makinda na
wakongwe, kwamba umakini, ujanja, wepesi alioufanya ni sehemu ya kufanya kwake
vizuri na kuweza kufunga.
Uamuzi wa
kuthubutu, pia ni jambo lililomsaidia Okwi kufunga. Angehofia lawama, basi
asingeweza kupiga mpira ule. Lakini aliamini angefanikiwa, akatenda na ikawa.
Wachezaji wengine wanaweza kujifunza kupitia yeye kwamba uthubutu ni kwanza,
halafu mafanikio yanafuata.
Bao la Okwi ni
bora, ubora wa bao hilo ni maswali ya soka ya Tanzania ilipofikia na washiriki
wake na kama kutakuwa na mabao mengi ya kiwango hicho, basi ni kipimo tosha
kuwa tumeanza kupanda.
0 COMMENTS:
Post a Comment