Mshambuliaji nyota wa Yanga,
Amissi Tambwe, amerejesha fadhila kwa kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, kwa kudai alisaidia kuokoa kipaji chake
baada ya kuidhinisha auzwe kwenda Yanga.
Tambwe aliuzwa na Simba
kwenda kuitumikia Yanga msimu uliopita, lakini usajili huo ulipigiwa kelele
sana na mashabiki wa soka wa timu hiyo huku kila mmoja akiamini kuwa Simba
hawakuwa sahihi kumuuza.
Hata hivyo, viongozi wa
Simba walikuwa wakitupiana mpira mara kwa mara huku kila mmoja akisema kuwa
hakuhusika kuuzwa kwa mchezaji huyo, lakini juzi Hans Poppe kupitia makala
iliyoandikwa na Gazeti maarufu la Michezo na Burudani la Championi, alisema
kuwa yeye ndiye alipitisha usajili huo ili kuokoa kipaji chake.
Hata hivyo, ingawa Tambwe
ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita alionekana kujiuliza
maswali mengi kuhusiana na kauli ya Hans Poppe akilinganisha na maisha halisi
aliyokuwa akiishi klabuni hapo, mwisho akaiunga mkono akitamka kuwa anashukuru
kwa hicho alichokifanya kwake maana sasa amerejea kwenye kiwango chake cha
awali na mambo yanamnyookea uwanjani.
“Nilikuwa silifahamu hilo
na siwezi kumbishia, ila kama alivyosema ninamshukuru, kweli nashukuru kwa
alichokifanya kwangu kwa ajili ya kuniokoa. Sasa hivi nipo Yanga nafanya vizuri
na nimeanza kurejea kwenye kiwango changu, nashukuru kwa kweli kama alivyokuwa
amesema, maana sijui ingekuwaje hapo baadaye.
“Unajua kocha anaweza
kukumaliza hivihivi kama ikitokea ameamua kufanya hivyo na wakati ule
nisingeweza kumbishia Phiri au kusema lolote kwa kuwa ananiweka benchi kwa
sababu yeye ndiyo mwamuzi wa mwisho, ila ndiyo hivyo Mungu naye anaona, kama
mtu anafunga mlango mdogo basi yeye anaweza kukufungulia mlango mkubwa na
ukanufaika zaidi,” alisema Tambwe ambaye mpaka sasa ana mabao matano kwenye
ligi.
0 COMMENTS:
Post a Comment