Kikosi cha Etoile du Sahel ya Tunisia, kililazimika kuganda
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa dakika 100
kukamilisha taratibu za uhamiaji na walipotoka uwanjani hapo walionekana wakiwa
na wapishi, vyakula na maji ya kunywa.
Klabu hiyo imefanya yote hayo ili kukwepa
hujuma kutoka kwa Yanga ambayo leo Jumamosi watacheza nayo kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar katika mechi ya Kombe la Shirikisho.
Kikosi cha Etoile kilitua uwanjani hapo saa
9:00 usiku wa kuamkia jana kwa ndege ya kukodi, lakini kilitumia muda mwingi
katika kukamilisha taratibu za uhamiaji na kutoka saa 10:40 alfajiri kueleka
Hoteli ya Ledger ambayo zamani ilifahamika kama Bahari Beach iliyopo Kunduchi,
Dar.
Waarabu hao walitua na msafara wa watu 56,
wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tunisia (FTF), Krifa Jalel na rais wa
klabu hiyo, Charefeddine Ridha. Wengine ni wachezaji 19, viongozi na watu wa
benchi la ufundi 13, waandishi wa habari 12 na mashabiki 10. Msafara huo
uliondoka uwanjani hapo na mabasi mawili na magari madogo manne.
Muda mfupi baada ya kutua, kiongozi mmoja wa
Etoile alimfuata mwakilishi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Raphael
Matola ili awasaidie wapewe kipaumbele kwa watu wa uhamiaji ili kukamilisha
taratibu lakini alikataa akiwataka kufuata utaratibu uliopo.
Ulipofika wakati wa kutoka, msafara wao
ulionekana kuwa na mizigo mikubwa ya vyakula mbalimbali na maji ya kunywa
ambapo ofisa mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mpishi alisema wamefanya hivyo ili
kukwepa hujuma.
“Tumekuja na kila kitu, hapa tuna maji na
chakula ambacho tutakula hadi siku tunaondoka, tumepanga kufanya vizuri,”
alisema ofisa huyo.
Maofisa wa Etoile waliwakataza wachezaji wao
kufanya mahojiano na vyombo vya habari na hata straika wao wa kutumainiwa,
Mualgeria, Baghdad Bounedjah alikataa kuzungumza akisema hafahamu Lugha ya
Kiingereza.
Alipotakiwa kuzungumzia mchezo huo kwa Lugha
ya Kiingereza, Baghdad alijibu kwa lugha hiyo: “Siielewi vizuri Lugha ya
Kiingereza, nafahamu Kifaransa kidogo, labda uongee na wenzangu.”
Hata hivyo, Baghdad alionekana akizungumza
Kiingereza safi na wenzake ndani ya basi dogo la Hoteli ya Ledger lililowafuata
uwanjani hapo. Alipoulizwa atafunga mabao mangapi kwenye mechi ya leo dhidi ya
Yanga, Baghdad alionyesha vidole vitatu akiwa na maana atafunga mabao matatu.
Alipofuatwa Kocha wa Etoile, Roger Lemeur,
alisema: “Mimi Kiingereza changu siyo kizuri, isitoshe nimechoka na safari hii
ndefu.”
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa
Yanga, Jerry Murro alithibitisha kuwa timu hiyo kuja na wapishi, vyakula na
maji ya kunywa.
0 COMMENTS:
Post a Comment