April 18, 2015



Na Saleh Ally 
JAMANI huku kugumu sana! Wengi mnaangalia nani atatwaa ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini mmepasahau kabisa huku.


Ninamaanisha mkiani, hali si nzuri na hakuna hata mmoja anayegombea ubingwa wa Ligi Kuu England. Kila upande unawania kuokoa ‘roho’ yake ili uendelee kubaki katika ligi kuu.

Timu tatu zitateremka, ambazo zimekalia mstari mwekundu ni Leicester City inayoshika mkia, Burnley iliyo katika nafasi ya 19 na QPR. Hakuna hata mmoja kati yao mwenye uhakika wa kubaki.

Maana tofauti ya pointi zao unaifanya kila timu kuwa na hofu kwa kuwa ikipoteza mechi moja tu, imejichimbia kaburi kabisa. Itakayoshinda moja au mbili, inachupa umbali mrefu.


Kuchupa umbali mrefu kutokana na timu nyingine tano baada ya hizo tatu kuonekana bado zinalazimika kupambana dhidi ya mstari mwekundu kwa kuwa zinaweza kuporomoka pia.

Timu hizo baada ya michezo kati ya 31 hadi 33, Newcastle, West Brom, Aston Villa, Sunderland, Hull City nazo zinaonekana hazina uhakika wa asilimia mia wa kuendelea kubaki Ligi Kuu England.

Huna haja ya kuhesabu mechi walizobakiza, lakini ukweli ndiyo huo kwamba timu iliyo katika nafasi ya 13 hadi 20, bado hazina uhakika hata kidogo kubaki Ligi Kuu England. 

Kuanzia juu kwenda mkiani Newcastle ina pointi 35, inafuatiwa na West Brom (33), Aston Villa (32), Sunderland (29), Hull City (28), QPR (26), Burnley (26) na Leicester City (25).

Inasomeka hivi, tofauti ya pointi kuanzia aliye katika nafasi ya 13 ya Ligi Kuu England hadi anayeshika mkia ni 10 tu. Hivyo, atakayepoteza mechi mbili akiwa katika nafasi ya 13, rahisi kufikiwa na aliye katika nafasi ya 20 kama atashinda tatu.

Ukiangalia katika timu hizo nane, mbili zinalingana pointi, tatu zinatofautiana pointi moja na mbili tofauti ni pointi mbili tu. Usisahau, baadhi ya hizo zitakutana zenyewe kwa zenyewe.

Huu ndiyo ugumu ulio mkiania katika Ligi Kuu England. Huenda upande huu ndiyo ukawa wenye presha kubwa maradufu kuliko upande mwingine wowote. Wengi huamini wanaowania ubingwa tu kama Chelsea, Arsenal, Manchester United na Manchester City ambao ni mabingwa watetezi ndiyo wenye presha kubwa pekee. La hasha!

Kinachofanya presha iongezeke zaidi, timu nyingi zilizo chini na zinazopambana kubaki, mwenendo wao hovyo kabisa. Katika mechi sita, Leicester walio mkiani wameshinda mbili, sare tatu na kupoteza mbili. Wanaowafuatia Burnley wameshinda moja, sare nne na kupoteza moja.

QPR walio katika nafasi ya 18, wameshinda moja, sare moja na wamepoteza nne. Halafu Hull City wamefungwa nne na sare mbili huku Sunderland wakiwa wamechapwa mara nne, sare moja na ushindi mmoja tu!

Mwenendo wa kusua ndiyo taswira sahihi kwamba kuna ugumu kwa timu hizo za mkiani, lakini ratiba nayo inawahukumu kwa kuwa wanakutana na timu zinazowania kubeba ubingwa wa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Basi inakuwa tabu tu!

Raha ya mkiani si kama kileleni. Huku si rahisi kuhakikisha kwamba Burnley imeshateremka. Ngoma bado ngumu na walio nafasi tatu za chini wana nafasi ya kuondoka na kuwaachia msala wengine.

Mechi zinaendelea leo, kesho na keshokutwa. Utaona kuwa kweli huku kugumu, atakayezubaa anaweza kuporomoka hata nafasi tatu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic