Habari ya Mbeya kwa sasa ni mechi ya Ligi Kuu Bara inayochezwa
leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Sokoine kwa kuzikutanisha Mbeya City na Simba.
Tayari mashabiki wengi wameonekana kuwa na
pilikapilika za mchezo huo huku kukiwa na kumbukumbu ya Simba kufungwa mabao
2-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Wakati Simba ikipambana kujihakikishia kufika
nafasi ya pili ikiwa na pointi 35 katika nafasi ya tatu, Mbeya City inapambana
kuhakikisha haiingii katika hatari ya kushuka daraja kwani ipo nafasi ya kumi
ikiwa na pointi 25.
Kocha wa Simba, Mserbia, Goran Koponuvic,
akizungumzia mchezo huo, alisema: “Huu ni mchezo mgumu kwangu, tunatakiwa
kupambana sana ili tupate ushindi, japokuwa hatutakuwa na Okwi (Emmanuel) kwani
mwanzo walitufunga hawa jamaa.”
Kwa upande wa Mbeya City, ofisa habari wa timu
hiyo, Dismas Ten, alisema kikosi chao kimeandaliwa vizuri na hakina hofu yoyote
dhidi ya Simba.
“Simba ni timu ya kawaida sana na tumejiandaa
kama tunavyojiandaa kucheza na timu nyingine za ligi kuu, tunahitaji pointi
tatu na wachezaji wote wako fiti kwa ajili ya mchezo huu,” alisema Ten.
0 COMMENTS:
Post a Comment