Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm ametazama video za mechi za
Etoile du Sahel na kusema amegundua kikosi chao kina tatizo la mabeki
wanaocheza taratibu mno.
Kutokana na kugundua udhaifu huo wa safu ya
ulinzi ya Waarabu hao wa Tunisia, Pluijm amepanga kuwatumia kwa pamoja mawinga
wenye kasi Simon Msuva na Mrisho Ngassa kuwachosha mapema wapinzani wao.
Katika mazoezi ya jana asubuhi kwenye Uwanja
wa Karume, Pluijm alionekana akitumia muda mwingi kuwaelekeza Msuva na Ngassa
jinsi ya kuiwahi mipira mirefu itakayokuwa ikipelekwa kwao na viungo.
“Inabidi tucheze kwa kasi sana, kwani mabeki
wa Etoile hawana kasi lakini washambuliaji wao wana kasi hivyo ni wazuri wakiwa
na mpira, sasa tutatumia udhaifu wao nyuma lakini lazima tujilinde kwa
washambuliaji wao,” alisema Pluijm raia wa Uholanzi.
Akizungumzia mchezo huo, Msuva alisema: “Nimejipanga
kufanya vizuri dhidi ya Etoile kwani kocha amenielekeza kuhusu nini cha kufanya
na natakiwa kukimbia sana katika kushambulia.”
0 COMMENTS:
Post a Comment