May 23, 2015



LONDON, England
UNAPOAMUA kuzungumza ukweli mara zote ni lazima utakuuma wewe unayezungumza au ukamuumiza yule au wale ambao unawasema, hasa kama ikiwa kwa mabaya au kwa kukosoa.


Thierry Henry ana jina kubwa ndani ya Klabu ya Arsenal na kila shabiki wa timu hiyo analijua hilo, inaaminika kuwa ndiye mchezaji bora kuwahi kutokea ndani ya klabu hiyo, kwa ufupi heshima yake ni kubwa klabuni hapo.

Pindi alipotangaza kustaafu kucheza soka na kuamua kuwa mchambuzi, wengi waliamini kuwa ipo siku lazima atakwaruzana na timu yake hiyo ya zamani na ndivyo inavyoanza kutokea.

Awali alipoanza kazi ya uchambuzi ndani ya kituo cha Sky, hakuwa mkosoaji mzuri, lakini muda mfupi baadaye akaanza kukosoa mambo mengi yakiwemo hata yanayoihusu Arsenal.

Gumzo ni juu ya kauli yake kuwa Arsenal haiwezi kutwaa ubingwa kwa kumtegemea mshambuliaji Olivier Giroud, alisema anaamini ni jambo zuri kwa kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger, kusajili straika wa kiwango cha juu kama kweli anahitaji ubingwa wa Premier.


Tangu Henry alipoondoka klabuni hapo, Arsenal haijawahi kutwaa ubingwa wa Premier kwa muda wa miaka 11, kumekuwa na sababu nyingi lakini hiyo ya kukosa straika mwenye kiwango cha juu inatajwa kuwa moja ya sababu kubwa.

Kuhusu hilo Wenger alijibu kuwa anajua mchezaji wake huyo wa zamani analipwa fedha nyingi na anapata presha kubwa kutoka kwa mabosi wake wa sasa ili aweze kukosoa na kutengeneza vichwa vya habari, ndiyo maana anatoa kasoro hizo.

Alichosema Wenger ni kweli, presha ni kubwa na hata fedha ni nyingi anayolipwa, lakini ndani ya nafsi yake anajua alichosema Henry kina ukweli.

Kwa asili ya Premier, ni jambo gumu kuona timu ikitwaa ubingwa ikiwa haina mshambuliaji wa kiwango cha juu daraja A. Mfano ni ilivyokuwa kwa Chelsea msimu uliopita, ilikuwa na washambuliaji wa kawaida, lakini safari hii ikamsajili Diego Costa kwa dau kubwa na ndiye aliyechangia ubingwa kwa kiwango cha juu.


Arsenal imekuwa ikipata tatizo la kutokuwa na straika daraja A kwa miaka mingi, angalau miaka ya hivi karibuni Wenger alikuwa akisajili wachezaji wa gharama kubwa tofauti na ilivyokuwa sera yake ya kutegemea chipukizi wa bei rahisi ili awakuze, ndiyo maana akapata taji la FA Cup na Ngao ya Jamii.

Giroud naye amemjibu Mfaransa mwenzake huyo na kuonyesha kupuuzia kile alichokisema, lakini akikaa chumbani kwake juu ya kitanda na kutulia, anaweza kuwa anaujua ukweli lakini tu hataki kuonyesha kuwa anaujua.

Kauli ya Henry, ambaye alifunga mabao 226 katika maisha yake ya Arsenal, ilikuwa hivi: “Nafikiri Giroud anacheza vizuri lakini unadhani unaweza kutwaa ubingwa kwa kumtegemea yeye? Sidhani kama inawezekana hiyo.”

Giroud, 28, anaelekea kumaliza msimu akiwa amefunga mabao 14 katika mechi 26 alizocheza baada ya kuwa nje kutokana na kuandamwa na majeraha kwa muda wa wiki kadhaa, hivyo kukosa mechi nyingi ndani ya msimu huu.

Arsenal inamaliza msimu huu ikiwa katika nafasi ya tatu nyuma ya Chelsea yenye Costa na Manchester City yenye Sergio Aguero, huku ikiwa mbele ya Manchester United yenye Robin van Persie na Radamel Falcao ambao hawakuwa kwenye kiwango kizuri.

Hali hiyo ya Falcao na van Persie inathibitisha kuwa ili ubebe ubingwa au ufanye vizuri, pamoja na kuwa na kikosi imara lakini straika wa kiwango daraja la kwanza na ambaye yupo kwenye kiwango kizuri ni muhimu zaidi.

Jina:            Olivier Giroud
Kuzaliwa:  Septemba 30, 1986
Alipozaliwa:       ChambĂ©ry, Ufaransa
Urefu:                           6 ft 4 in
Nafasi:                 Mshambuliaji
Jezi:                     Namba 12


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic