Na Maulid Kitenge, Tunisia
WAKATI mpira ukiwa
unabadilika duniani, Waarabu bado wamejaa kasumba ileile ya kizamani ya mambo
ya ajabu kabla ya mchezo.
Niko mjini Tunis, Tunisia
kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Yanga na wenyeji wa hapa, Etoile du Sahel,
itakayopigwa kesho usiku mjini Sousse lakini nilichokiona sikuamini.
Nikajiuliza, hivi kwenye karne hii mambo haya ya fitna za Kiarabu bado yapo?
Kwanza wamewagandisha Yanga
uwanja wa ndege kwa saa mbili, wakisema wanashughulikia viza lakini kilichokuwa
kinafanyika kilikuwa hakionekani mpaka msafara wa Yanga ulipoamua kuchachamaa
na kupiga kelele, ndipo wenyeji walipoharakisha kushughulikia suala la viza.
Nikajiuliza hivi mpaka watu wapige kelele?
Timu kubwa kama Etoile du
Sahel ambayo tayari ina rekodi ya aina yake barani Afrika ya kunyakua karibu
makombe yote, sikutegemea kama itafanya ubabaishaji wa aina hiyo. Nilijua kama
walikuwa wanafanya, basi zamani na siyo sasa.
Hivi dunia ya leo
ukamgandishe mgeni wako uwanja wa ndege ‘airport’ ili umuondoe mchezoni!
Lakini kituko kingine
kilikuja wakati timu ilipotoka uwanja wa ndege na kukumbana na gari lililoandaliwa
na wenyeji hao, eti Toyota Coaster ambayo imechoka, kwamba hiyo ndiyo Yanga
wafanye nayo safari ya saa moja na nusu kuelekea mjini Sousse ambako kutachezwa
mchezo huo wa marudiano kesho Jumamosi.
Bahati nzuri kumbe Yanga
walishajiandaa wakawa wamekodi basi kubwa na lile Toyota Coaster ambalo
liliandaliwa kwa ajili ya wachezaji tukapanda akina sisi.
Wakati nikiwa nimekaa
kwenye gari hilo lililochakaa, nilikuwa najiuliza; kumbe ndiyo maana Afrika
tukienda Kombe la Dunia hatufiki mbali! Na kwa hali hii tunastahili tusifike
mbali, maana bado kasumba za hujuma za kizamani tunazo wakati wenzetu Wazungu
hawana mambo haya.
Sasa kama miamba Etoile
wanafanya mambo kama haya, timu ndogo za Afrika nazo zitajifunza nini? Nilichojifunza
ni kwamba sisi Watanzania tumekuwa wakarimu sana. Ipo haja sasa nasi kufanya
mambo kama haya kwa vile timu zetu ugenini zinafanyiwa.
Siku zote Watanzania, klabu
hata za Waarabu zinapokuja kucheza soka nchini, huwa tunazikarimu sana wakati
sisi tukienda kwao tunafanyiwa vitendo vya ajabuajabu.
Kama tunataka kushindana
nao, basi angalau japo kwa muda tuwe na sisi tunauweka ubinadamu kando ili
tuwachanganye kama wanavyotuchanganya sisi. Tuwaondoe mchezoni kama wao
wanavyotuondoa sisi mchezoni.
Kama tusipofanya kama wao
wanavyotufanyia, bila shaka hatuwezi kushindana nao na kuwatoa, kwa kuwa wao
wanaweza wasituzidi uwezo uwanjani, bali wanatuzidi hujuma za nje ya uwanja.
Lakini kwa namna yoyote
ile, mambo kama haya tunapaswa kuyakemea kwa kuwa yanaua soka letu. Nchi za
Afrika haziwezi kufanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa kuwa
zinategemea sana hujuma, kitu ambacho siyo sawa.
Kwa kuwa Waarabu hawataki
kusikia, basi nasi tuzibe masikio kwa pamba, tukikutana nao basi iwe jino kwa
jino ili tuende nao sawa.
Vinginevyo tutakuwa
tukitupwa nje ya michuano tukikutana nao wakati pengine uwezo wa uwanjani
tunao, tena kuliko hata wao.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment