KIKOSI cha Yanga kimewasili nchini Tunisia kwa ajili ya
mechi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya wenyeji wake, Etoile du Sahel.
Mechi ya kwanza mjini Dar es Salaam, timu hizo mbili zilitoshana
nguvu kwa sare ya bao 1-1, Waarabu hao wa Tunisia wakisawazisha kipindi cha
pili.
Yanga wanatakiwa kushinda au sare ya aina yoyote ile
kuanzia 2-2 ili kuweza kusonga mbele. Wote tunajua haitakuwa kazi rahisi hata
kidogo kwa Yanga kuuvuka mlima wa Waarabu hao.
Nawaita mlima kutokana na kazi ngumu wanayotakiwa
kuifanya Yanga. Wapande vipi, nguvu yao ikoje na wapinzani wanaokutana nao wako
vipi.
Kazi hiyo inatakiwa ifanyike kesho, Etoile wamejiandaa
na wameonyesha kwamba mambo yao wanayafanya kwa tahadhari kubwa wakiamini Yanga
si timu ya kubeza.
Wote tuliona timu yao si ya kubahatisha, ni washindani
hasa kwa Yanga na wana wachezaji wengi wa viwango vya juu kuliko hata wale wa
Yanga, hakuna haja ya kuficha.
Tuliona
wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, walionyesha soka
safi, soka la mipango na walionekana ni watu walioiva kwa ajili ya michuano ya
kimataifa. Haitakuwa kazi rahisi kwa Yanga, lakini si kazi isiyowezekana kwa
asilimia mia.
Kweli mpira una maajabu yake, lakini Yanga hawawezi
kukaa, wakasinzia halafu maajabu yakafanya kazi yenyewe. Lazima wapambane kweli
wakijua kazi waliyonayo ni ngumu zaidi ya ile waliyokutana nayo jijini Dar es
Salaam.
Baada ya sare, asilimia 50 ya watu wa Yanga wakiwemo
mashabiki walikata tamaa kabisa. Nilizungumza na baadhi ya wachezaji wa Yanga,
ingawa mazungumzo yao yalionyesha wanaweza kufanya maajabu na watapambana,
lakini hakukuwa na mwendo mmoja kati ya macho na matamshi yao.
Hata wao walionekana kuwa na hofu, jambo ambalo
ninaamini ni baya zaidi kwa Yanga kwa kuwa kama watakwenda na hofu kwamba jamaa
hawawezekani, basi ni rahisi sana kufungwa hata bao tano au saba.
Watu wa mpira, tano wanaita mkono na saba ni wiki. Kweli
kabisa, kama Yanga wataamini hawawawezi Etoile kabla ya kuingia uwanjani,
lazima wajue wanajitengenezea chumba cha kupigwa mabao mengi na kuingia katika
aibu. Badala yake wanapaswa kujua wao sasa ni wawakilishi wa Yanga na taifa
pia.
Hivyo lazima wapambane mwanzo mwisho na kwa juhudi na
ufundi wa juu na hapo ndiyo soka linaweza likaleta maajabu yanayoweza kutokea
na kufanya kazi yake.
Waungwana, kweli Etoile wana uwezo mkubwa. Tukubali hata
Al Ahly nao ni wakubwa, tena kuzidi timu hiyo ya Tunisia, lakini tuliona
walivyopata kazi kubwa kwa Yanga hadi kuwatoa kwa mikwaju ya penalti, tena
Yanga wakiwa na nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele.
Timu za Waarabu ni bora kuliko zetu kutokana na mazingira
na hali halisi lakini katika soka mara nyingi umeona timu iliyoonekana haiwezi
kushinda, ikifanya hivyo kwa kuwa watu walijiandaa na walipambana kiume.
Hata kama wanawake wanacheza, soka ni mchezo wa kiume.
Wanaume jasiri hawarudi nyuma, badala yake wanapambana hadi tone la mwisho.
Yanga inaweza kupambana na kufanya vizuri dhidi ya Etoile.
Yanga haikuwa na mchezo mzuri katika mechi ya kwanza
jijini Dar es Salaam. Inaweza ikawa na mchezo mzuri ugenini huku Etoile nao
wakiwa hawana mchezo mzuri nyumbani. Hayo yote ni mambo ya mpira na yanatokea.
Yanga hawapaswi kuangalia uzuri au ubaya wa mchezo, muhimu kupambana wakiwa na
malengo.
Kitu cha kwanza ni kukubali ni mechi ngumu, pili ni
maandalizi ambayo yamefanyika, tatu ni kufuata maelekezo ya mwalimu, nne ni
kuamini inawezekana na tano ni kupambana hadi kieleweke. Kila la kheri.
0 COMMENTS:
Post a Comment