May 25, 2015


Na Saleh Ally
 ULIMUONA Xavier Harnandez I Crueus akimwaga chozi wakati akiwaaga mashabiki wa Barcelona? Liite chozi la chuma.


Jiulize kiungo huyo nyota wa Barcelona, Hispania na maarufu duniani kote analilia nini sasa? Nini kakosa au nini hasa sasa katika mapenzi yake ya soka au maisha ya kawaida?

Wahispania wamembatiza jina la kuwa ndiye mchezaji bora zaidi wa kiungo kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha miaka ishiriki.

Kwa Kihispania wanasema “Mejor de la historia” au “best ever” kwa Kiingereza. Ndiye kiungo ambaye amepata kila taji ambalo mchezaji anastahili kulipata.

Akiwa na Barcelona, Xavi amebeba mataji 23 yanayotambulika, akiwa na kikosi cha timu ya taifa amechukua mataji manne makubwa kwa ngazi za bara na dunia.



Ametwaa mataji nane ya La Liga, mawili Copa del Rey, Super Cup ya Hispania sita, amechukua ubingwa wa Ulaya mara tatu na mataji mawili ya Uefa Super Cup, pia usisahau ubingwa wa dunia kwa klabu, mara moja.

Akiwa na timu ya taifa amechukua makombe yote muhimu ambayo ni Kombe la Ulaya mara mbili, Kombe la Dunia la vijana mara moja kama ilivyo kwa Kombe la Dunia.

 Ukiangalia utagundua Xavi alikuwa ni ‘roho’ ya Barcelona na Hispania kwa kuwa pamoja na kucheza mechi nyingi sana lakini hakufunga mabao mengi.

Xavi amecheza jumla ya mechi 567 akiwa na Barcelona, lakini akafunga mabao 57. Unaweza ukashangazwa kwamba kwa misimu 17 amefunga mabao hayo tu?


Lakini pia unaweza ukajiuliza, kwa mabao hayo machache vipi amekuwa ni mchezaji kwenye kikosi chenye mafanikio kibao kwa miaka hiyo 17? Hata katika timu ya vijana ya Barcelona, pamoja na kucheza kwa misimu mitatu akiwa ameshuka dimbani mara 61, alifunga bao moja tu kwa misimu yote mitatu!

Kiasi fulani inashangaza, lakini jibu lake lipo. Kwamba Xavi hakuwa mfungaji, badala yake ndiye ‘roho’ ya timu ambaye alikuwa akiunganisha uhai wa wachezaji wengine wote uwanjani.

Kuwepo kwake, kiungo kinaungana na difensi na kiungo kinaungana na washambuliaji. Kufunga kwake halikuwa jambo muhimu sana.


Hivyo kama utazungumzia suala la mabao, basi ni pasi za mabao ndiyo zilikuwa kazi yake. Hii inaonyesha kiasi gani ni kati ya wachezaji waliojitambua na walikuwa wakijua nini hasa kinawafanya wawe uwanjani.

 Ndiye aliyekuwa akipewa jukumu la kuifanya timu itembee au kutulia. Karibu kila mpira alipewa yeye kuituliza timu wakati inashambuliwa sana au inapokuwa inashambulia zaidi.

Mipango ya wafanye nini ili wafunge ilianzia kwake. Hii kazi aliifanya kwa makocha karibu wote ambao wameifundisha Barcelona.


Msimu huu uliomalizika juzi, Xavi akiwa na miaka 35 ameonekana kuporomoka kwa kuwa amecheza mechi 31, akiwa ameanza 19, ameingia 12 na kutolewa katika mechi 10.

Xavi ni mchezaji ambaye anaweza kutumika kuwakumbusha Hispania, bara zima la Ulaya lakini Tanzania na ikiwezekana bara zima la Afrika.

Xavi alikuwa staa hasa, mchezaji aliyepata mafanikio makubwa sana kuliko hata wengi maarufu duniani.

Ameingia katika listi ya wachezaji waliowahi kuchukua taji la mchezaji bora wa Dunia mwaka 2010, lakini ilikuwa si rahisi kumsikia ameingia kwenye mzozo.

Haikuwa rahisi kumsikia Xavi ameongozana au kuzozana na mwanamke ambaye si mpenzi wake. Si rahisi kusikia anazozana na kocha fulani.

Wakati mwingine hata uwanjani, ilikuwa ni nadra sana kuzozana na wachezaji au waamuzi. Ni mchezaji ambaye amejitambua tokea mtoto, kijana na mtu mzima pia.

Anaondoka Hispania baada ya misimu 17 akiwa na Barcelona ya vijana na ile ya wakubwa. Lakini kila utakachosikia kuhusiana na yeye ni ubora wa kazi yake na si skendo.

Wachezaji wangapi leo hawana hata robo ya robo ya mafanikio ya Xavi, lakini wameishavimba vichwa? Wangapi ambao wako Yanga na Simba na wanaona ndiyo mwisho wa safari yao?


Xavi anastaafu ndiyo anakwenda kumalizia miaka yake mitatu katika klabu ya Al Asaad ya Qatar huku akijazwa mamilioni ya fedha kuwa balozi wa Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022.

Kama wewe uliye na kidogo umeshavimba kichwa? Xavi atakufa kabisa! Inawezekana kabisa ukajifunza mengi, kwamba hata kama si Mtanzania au yuko mbali, bado kuna nafasi ya kuangalia alikopita.

Xavi hakuwa bora uwanjani tu, kwani hata nje ameonyesha mfano kwamba yeye ni kiungo bora kabisa, baba au mzazi wa kiwango cha juu na mwenye familia iliyo na utulivu na mambo yanawezekana ili mradi ukibali kujifunza. Angalau chukua hata vichache kutoka kwake, hakika utapata mabadiliko.

Heshima anayoondoka nayo, si rahisi kuipata kwa ujanja ujanja. Amini inawezekana hata robo yake, lakini pia ukubali lazima iwe kazi ya ziada.

Si rahisi kujilinganisha naye kila kitu kwa kuwa watu kama yeye ni wachache sana duniani. Lakini unaweza kutengeneza kitu bora kwa kujipima namna ubora wake ulivyotengenezwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic