SHIRIKISHO la
Soka Tanzania (TFF) ndilo lenye jukumu la kuisimamia timu ya taifa, Taifa Stars
ambayo ni mali ya Watanzania.
Jukumu hilo
linaendana na mambo mengi kwa kuwa TFF wanalazimika kuhakikisha timu hiyo
inapata kila kinachohitajika ili mambo yaende vizuri.
Kwa sasa mambo
hayaendi vizuri na hata TFF wanalijua hilo, kuwa mambo si shwari hata kidogo na
Watanzania hatuna raha na timu yetu.
Kocha Mart Nooij ameyumba
kwa kiasi kikubwa. Hajaonyesha njia sahihi ambayo inaweza kuisaidia Taifa Stars
katika mambo mengi, ndiyo maana wadau wanapiga kelele ya kutaka aondoke.
Mimi naungana na
wale wanaotaka aondoke, licha ya kuwa TFF nao wametoa hoja zao kwamba kama akiondoka
katika kipindi hiki, itakuwaje kuhusiana na suala la mechi nyingi zinazokuja
kuwa karibu.
TFF wanaona ni
sahihi kumbakiza Nooij kwa kuwa mechi inayofuata dhidi ya Misri ni wiki mbili
zijazo.
Baada ya hapo, ndani ya wiki mbili tutacheza na Uganda mara mbili,
usisahau pia mechi ya Nigeria. Hadi Septemba 10, kutakuwa na mechi zaidi ya
nne. Hiyo ndiyo hofu ya TFF kwamba kama atakuja kocha mpya, itakuwa ni vigumu
sana kuwajua wachezaji na kuanza kukipanga kikosi kilivyo! Lakini huenda
wangewatumia makocha wazawa kusaidia kumuongoza mgeni.
Wakati TFF bado
wanapambana na hili la kumbakiza au kumuondoa Nooij, uchunguzi nilioufanya
ndani ya shirikisho hilo, inaonekana kumekuwa na matatizo makubwa ya ulipwaji
wa fedha za udhamini kutoka kwa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
TBL kupitia bia
yake ya Kilimanjaro ndiyo wadhamini wakuu wa Taifa Stars na tunapaswa
kuwapongeza kwa kuijali timu yetu ya taifa.
Hiyo ndiyo timu namba moja ambayo
inawaunganisha Watanzania wote wanaojitambua na kuipenda nchi na michezo kwa
dhati.
Kampuni
inayojitokeza kuidhamini timu ya taifa, inapaswa kuthaminiwa. Lakini nimegundua
kuna tatizo kubwa unapofikia wakati TBL kutakiwa kuilipa TFF fedha kwa ajili ya
maandalizi fulani ya timu ya taifa, jambo ambalo limekuwa likisababisha
matatizo makubwa.
Mara kadhaa, TFF
wamekuwa wakilazimika kukopa kutokana na TBL kuchelewesha malipo yao. Yaani
hawafuati mkataba unavyoeleza, jambo ambalo si sahihi na linaweza likawa
linachangia pia kuua morali ya wachezaji.
Taifa Stars
iliwahi kuwa katika mgogoro mkubwa na wamiliki wa hoteli moja nchini Zimbabwe,
kwa kuwa walikwenda kwa kubangaiza kwa sababu TBL walichelewesha kuwapa malipo
yao.
Safari hii Taifa Stars
imeboronga kwenye Michuano ya Cosafa kwa kufungwa mechi zote na hakika Nooij ni
namba moja katika hili kwa kuwa timu ilishindwa kuonyesha kiwango, ikaondoka
Afrika Kusini bila ya kufunga hata bao moja.
Wakati
tunapambana na Nooij, nataka na TBL nao wajipime kwamba pamoja na kuwa
wadhamini wanaosaidia, mwisho wanaweza kuwa sehemu ya anguko la timu hiyo, kwa
kuwa wanaonekana kwa mara ya pili au tatu sasa wanashindwa kulipa fedha kwa
wakati mwafaka.
Mara mbili
nimeelezwa mwishoni mwa Aprili ndiyo ulikuwa wakati mwafaka wa TBL kulipa fedha
zake za udhamini. Haikufanya hivyo na Taifa Stars ikaondoka kwenda Afrika
Kusini kwa kujichanga ‘kiaina’.
Hakukuwa na
nafasi ya kuwapa wachezaji angalau motisha ya kutosha kwa kuwa hata posho TFF
walilazimika kujichanga. Jiulize kama TBL wao ni wadhamini, vipi wanaona ugumu
kutoa fedha hizo hadi waingie katika mzozo na TFF?
Lengo lao hakika
ni kujitangaza, lakini kama watawahisha fedha ambazo hawana sababu ya
kuzichelewesha hawaoni wanaweza kusaidia ufanisi wa Taifa Stars? Au hawajui
kuendelea kuicheleweshea malipo ni kuendelea kuizorotesha? Vipi wao wanaona
sahihi kudhamini kitu kinachozorota huku wao wakiwa wanachangia?
Itakuwa vizuri
sana TBL wakabadilika katika hilo ili kujiepusha kuunganishwa kwenye kundi la
wale wanaoizorotesha Taifa Stars kama ambavyo tumeona kwa kocha huyo Mzungu
ambaye anaonekana hajui kilichomleta Tanzania.
Lengo la TBL ni
kujitangaza kwa uzuri, sasa kama wataendelea hivi, mwisho watakuwa eneo la
tatizo na mwisho watashindwa kujitangaza wanavyotaka.
0 COMMENTS:
Post a Comment