| BAHANUZI WAKATI AKIITUMIKIA YANGA. |
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi, amesema kuwa
anatarajia kuifikisha mbele ya vyombo vya sheria klabu yake hiyo kufuatia
kukatishwa mkataba wake bila ya kulipwa kitu chochote.
Mchezaji huyo ambaye aliwahi kuchukua tuzo ya mfungaji bora ya
michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2012, akiwa na Yanga, mambo yalikuwa si mambo kufuatia kutopata nafasi ya
kucheza katika kikosi cha kwanza, amesema kuwa ataifikisha mahakamani klabu
yake hiyo iwapo haitajibu barua yake.
Bahanuzi ni miongoni mwa wachezaji saba waliotupiwa virago vyao
Yanga pamoja na Omega Seme, Thabiti Abdul, Anthony Matogolo, Danny Mrwanda,
Jerryson Tegete ambao bado hawajamaliza
mikataba yao pamoja na Nizar Khalfan ambaye mkataba wake uliisha.
Bahanuzi ambaye aliichezea Polisi Moro kwa mkopo msimu uliyopita,
alisema kuna mwanasheria ambaye anafanyanaye mazungumzo na kuupitia upya
mkataba wake ili kuweza kujua nini kimejiri kisha kuandika barua na kuiwasilisha
Yanga ili kuweza kupata majibu juu ya malipo yake.
“Nimepata barua ya kuachwa
na Yanga Mei 21 ambayo inaonyesha kuwa wamevunja mkataba na hawatahusika juu ya
kunitafutia timu nyingine kwa ajili ya kuichezea msimu ujao, jambo hilo
limenifanya kutopata timu hadi sasa kwa kuwa ilikuwa kama siri, hawakutangaza
kama ilivyo kawaida, hakuna timu inayojua kama nipo huru.
“Leo (Jumatatu), natarajia kukutana na mwanasheria wangu hapa
nyumbani kwa ajili ya kuupitia upya mkataba kisha kuangalia dosari ili kuweza
kujua nini kimetokea kisha tutawaandika barua kwa ajili ya kuipelekea klabu ambapo
tutaisubiria ndani ya siku kumi hadi 15 kupata majibu.
“Na iwapo hawatatujibu ndani ya siku hizo, itabidi nilifikishe
mbele ya sheria suala hili ili niweze kulipwa haki zangu kwa kuwa wao ndiyo
wamevunja mkataba na mimi,” alisema Bahanuzi.
Kuhusiana na suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha,
alisema: “Hatutahusika na suala la kuwatafutia timu wachezaji hao kwa kuwa kuna
kipengele fulani ambacho kipo ndani ya mikataba yao, ambacho kinaeleza
kuwa iwapo hatacheza katika kiwango
tulichokubaliana tunaachana naye, hivyo hatutahusika na kuwatafutia timu
nyingine wachezaji tuliowaacha.”
SOURCE: CHAMPIONI







Alitakiwa kujua amekutana na wasomi, muda wa kubweteka na kusubiria mishahara ya bure huku hujitumi umekwisha
ReplyDelete