Mshambuliaji wa Yanga anayeaminika kwa nguvu
nyingi, Kpah Sherman, amefunguka kuwa yupo tayari kuondoka klabuni hapo iwapo
tu klabu yake itataka kumtoa kwa mkopo.
Hivi karibuni imeripotiwa kuwa, Yanga wapo kwenye
mchakato wa kumtafutia timu watakayompeleka kwa mkopo baada ya kutoridhishwa na
kiwango chake msimu uliopita.
Akizungumza kutoka kwao Liberia jana,
Sherman alisema kuwa katu hawezi kuwakatalia kama wataamua hivyo, lakini ni
mpaka arejee kwanza klabuni kwake na kuangalia hali halisi.
“(Anacheka), sina taarifa hizo lakini kama
ni hivyo watataka niondoke, sawa tu maana yatakuwa ni maamuzi yao. Lakini ni
mpaka nikirudi Dar kuangalia hali halisi ya mambo yenyewe.”
Wakati huohuo, wakala wa nyota huyo wa zamani
wa Cetinkaya ya Cyprus, Gibby Kalule, alisema kuwa tayari kuna timu zimeonyesha
nia kumhitaji lakini kikwazo kikubwa ni mkataba wa miaka miwili alionao na
Yanga.
“Kuna timu zinamhitaji na mojawapo ni Bec
Tero ya Thailand, ambayo ndiyo mpya katika timu zilizovitiwa naye, lakini
hakuna kilichofanyika kutokana na mkataba wake na Yanga kuwa hai. Kama ikitokea
ameruhisiwa, chaguo la kwanza itakuwa ni hiyo,” alisema Gibby.
Wachezaji wengine ambao wanatajwa kuwa
kwenye mipango ya kupelekwa kwa mkopo ni Hassan Dilunga na Charles Edward ambao
wote wanatajwa kutakiwa na JKT Ruvu.







0 COMMENTS:
Post a Comment