Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, ametamba kwamba kwa maandalizi anayoendelea nayo sasa, yainaipa Yanga nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Kagame, ikiwezekana hata kutwaa ubingwa.
Yanga ni moja ya timu zitakazoshiriki
kwenye michuano hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 11, mwaka huu
jijini Dar es Salaam.
Pluijm amesema mara kadhaa amekuwa
akiulizwa kuhusiana na maoni juu ya timu yake katika Kagame lakini sasa anaona
bora awatoe hofu mashabiki wa timu hiyo kwamba yeye pamoja na kikosi chake
hakuna michuano wanayoihofia na kwamba wanafanya kazi moja tu ya kupambana na
kuchukua kombe.
Aidha, Pluijm aliongeza kuwa timu yoyote
inayotambua kuwa ipo kwa ajili ya kushindana, haiwezi kuwa na hofu.
“Najua kuhusu hii michuano na
ninafahamu kuwa wapenzi wa Yanga wanalihitaji hili kombe pia, lakini nikwambie
tu kwamba hata sisi tunajipanga na maandalizi yetu ya sasa pia yanajumuisha
hiyo michuano, kwa hiyo watu wasiwe na wasiwasi, tutakwenda kupambana kwa ajili
ya kuchukua kombe na si kingine.
“Kwa timu yoyote inayohitaji mafanikio
na kujua inahitaji nini lazima ijipange na kwenda kulitafuta hilo kombe kama
ilivyo kwetu Yanga, tutapambana kwa kuwa shida yetu ni hilo kombe na si
kingine,” alisema Pluijm aliyeiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara
katika msimu uliomalizika hivi karibuni.







0 COMMENTS:
Post a Comment