Na Saleh Ally
MWAKA 1993 nilifanikiwa kumuona Abbas Gulamali
kwa mara ya kwanza uso kwa uso. Alikuwa mtaani kwetu, kwa ajili ya kufanya
mazungumzo na baba yake mdogo Edibly
Lunyamila aitwaye Emmanuel Katamba.
Lengo lilikuwa ni kumalizia mazungumzo, kumsajili
Lunyamila kutoka Shinyanga Shooting kwenda Yanga. Nikiwa na ‘masela’ wengine wa
mtaani, tulijazana dirishani na kusikiliza nusu ya sehemu ya mazungumzo, kabla
ya kushitukiwa na kutimuliwa, halafu mlinzi akakaa kulinda dirisha
tusichungulie tena.
Lakini nina uhakika hata ukimuuliza Lunyamila leo
atakuambia, Lunyamila alisajiliwa kwa kitita cha Sh milioni 1, hilo ndilo
lilikuwa dau kutoka Shinyanga Shooting kwenda Yanga!
Wakati alipojiunga Yanga, kamwe hakuna mchezaji
aliyekuwa akilipwa mshahara licha ya timu hiyo kuwa na nyota kadhaa kama Issa
Athumani na Sanifu Lazzaro ‘Tingisha’.
Mwaka 1995, Lunyamila aliondoka Yanga na kujiunga
Malindi kwa dau kubwa la Sh milioni 3.5 akiweka rekodi kwa kumzidi Nico Bambaga
ambaye alisajiliwa kwa Sh milioni 3. Wote wakaanza kula mshahara wa Sh 15,000
kwa mwezi.
Mwishoni mwa mwaka, Lunyamila na Bambaga
walirejea Yanga baada ya Malindi kuvurugika, Wazambia kama Mordon Malitoli
wakarudi kwao. Lunyamila aliiendelea kuwa nyota, shujaa na mwisho mwaka 1998
aliisaidia Yanga kufuzu kucheza Klabu Bingwa Afrika hatua ya makundi baada ya
kuifunga Coffee ya Ethiopia ambayo ilikuwa imeing’oa Al Ahly ya Misri.
Baada ya ushindi huo, Kampuni ya MIC Tanzania
maarufu kama Buzz ikajitokeza kuidhamini Yanga chini ya uongozi wa Abbas Tarimba
kama sijakosea. Ikaanza kuvaa Simu Poa, wachezaji wa Yanga wakapata neema na
kwa mara ya kwanza wakaanza kulipwa mshahara wa Sh 60,000 kwa mwezi.
Kabla walikuwa wakilipwa fedha za mapato ya geti,
timu ikishinda wanapata zaidi, sare angalau na wakifungwa wakati mwingine,
hakuna kabisa.
Siku chache zilizopita nilipoandika kuhusiana na
wachezaji wa sasa kudai fedha rundo za usajili na mshahara huku wakiwa
hawajatoa msaada wowote kwa timu zao, wako waliolaumu sana, kwamba siwatetei
wachezaji.
Kamwe sihitaji kuwa shujaa kwa kuwatetea
wachezaji, au jabali la kuwapinga, lakini naendelea kusimamia kwenye haki kwao,
pia klabu zao kwa kuwa wote ni wadau wanaoweza kuukuza mpira au kuumaliza
kabisa.
Nataka uangalie vizuri, sasa ni miaka 10 imepita
tangu Lunyamila aliporejea Yanga akiacha mshahara wa Sh 15,000 kwa mwezi kutoka
Malindi. Miaka mitatu baadaye angalau akaanza kupata mshahara wa Sh 60,000
ambao wakati mwingine walilipwa baada ya miezi mitatu.
Ramadhani Singano wa mwaka 2015, anahitaji
kulipwa Sh milioni 60 za usajili, mshahara Sh milioni 2, safi, ni mzalendo
wacha afaidike, lakini tukirejea katika kazi yake, ameifanyia nini hasa Simba?
Hajaipa hata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa au ubingwa wa Nani Mtani
Jembe unaweza kuwa mafanikio makubwa sana?
Nataka uangalie uwezo wa Lunyamila yule miaka 10
iliyopita, anzia kwa Singano, nenda kwa Simon Msuva, mchukue Mrisho Ngassa,
halafu jiulize, tunapiga hatua mbele au tunarudi nyuma.
Ubora wa Lunyamila wa miaka 10 iliyopita, bado
uko juu maradufu ya wachezaji wetu wengi nyota wa sasa. Chukua makinda na
wakongwe, kwa huruma ya kizalendo, wote tunawapigia kelele walipwe vizuri
tukiamini watafanya vizuri zaidi!
Saleh Ally anayesema ukweli anaweza kuonekana ni
chenga tu, lakini ukweli utabaki palepale kuwa kama tunakuwa na Lunyamila bora
miaka 10 iliyopita, halafu miaka 10 baadaye tunakuwa na rundo la wachezaji
wasiofikia uwezo wake, tunafikiri tunaweza kupiga hatua?
Aliyekuwa hapewi mshahara alikuwa bora, hatari,
tishio hakuna mfano. Hii pia unaweza kuiona hata ukiangalia makipa wa sasa,
mabeki wa sasa na hata viungo wa sasa, jaribu kutafuta kiungo wa Tanzania
mwenye kariba ya Issa Athumani Mgaya, Hamisi Gaga ‘Gagarino’, Method Mogella
‘Fundi’, tumia muda wako wa kutosha, halafu niambie kiungo unayemjua sasa
mwenye uwezo huo.
Kama yupo utaniambia, kama hayupo nitakuuliza kwa
nini na kuna sababu ipi sasa ya wachezaji wetu kulipwa mishahara mikubwa? Ni
fasheni tu, au timu zinataka kuonyesha uwezo wa kifedha tu?
Okwi wa leo tunayemshangaa ni sawa na Lunyamila
wa mwaka 2005 ambaye alikuwa anaelekea kumaliza soka lake.
Wachezaji wamewahi kujipima kwamba uwezo walionao
wao sasa ni mdogo kuliko ule waliokuwa nao akina Said Mwamba ‘Kizota’ enzi
zile?
Kuna tatizo kubwa, wachezaji wajipime, vizuri
walipwe vizuri lakini nao lazima wajikague na kuangalia kiasi gani wanazilipa
klabu zao, wamezipa mafanikio gani nyumbani na kimataifa. Si kulialia tu kama
Ndorobo huku mkononi wana buku na wanataka mzigo wa Sh elfu 64.
Miaka 20 iliyopita kwa story yako ya kina Lunyamila na siyo miaka 10
ReplyDeleteuko sawa sana kaka Saleh, asiyekubali kubali huyo .com, ni ngumu sana kupata wachezi kariba ya kina Method Mogella "fundi", Justin Nicodemus Mtekere, Keneth Pius Mkapa, na wengine wengi tu wa maskani kina Joseph Lubisha, Masolwa n.k
ReplyDeletempira wa sasa ni fasheni tu hakuna kitu, mtu kama Singano kiwango chake ni chakawaida sana tena sana, asingeweza weza kucheza na watu kama David Mwakalebela au Kasongo Athuman Mgaya!!!
Na kiukweli tusipokuwa wakweli tutazidi kulitumbukiza soka letu shimoni siku hadi siku.
That's true brother Saleh, nakumbuka viwango vya akina Edward "Edo Boy"Chumila, Malota Soma"Ball Juggler", Hussein Amani Marsha, George Masatu, hawa ni baadhi tu ya wachezaji ambao waliweza hata kuifikisha Simba mbali kwenye michuano ya kimataifa. Viwango vyao, nidhamu zao, mapenzi pamoja na kujituma ndio kulikowajengea majina na kuwa wachezaji bora ambao mpaka sasa Tanzania haijaweza kuona wachezaji wa aina hiyo. Tunafahamu kuwa kwa wachezaji vipaji vyao ndivyo vinavyowawezesha kuendesha maisha yao pamoja na familia zao, ila wanatakiwa pia kuelewa ili uweze kuwa mchezaji bora na kustahili kulipwa mamilioni inabidi kuzingatia nidhamu, kujituma na pia uwe na uchu wa kujiendeleza na sio kuridhika na kubweteka.
ReplyDelete