Baada ya kukishuhudia kikosi chake kikipambana na timu ya
ushindani ya SC Villa kutoka Uganda, Kocha wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr,
amesema kwamba bado hajakiona alichokikusudia, hivyo anahitaji wiki tatu mpaka
nne ambazo ni sawa na siku 28, kwa ajili ya kurekebisha mambo kikosini kabla ya
kuanza kwa Ligi Kuu Bara Septemba 12, mwaka huu.
Simba ilivaana na Villa juzi Jumamosi na kuibuka na ushindi wa bao
1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, hiyo ikiwa baada ya kushinda michezo ya
kirafiki mfululizo ilipokuwa visiwani Zanzibar, lakini sasa Kerr amesema bado
anahitaji kutengeneza baadhi ya vitu ndani ya wiki hizo ambazo ni sawa na siku
28 kabla ya kuanza mshikemshike wa ligi kuu.
Kerr hakutaka kuwa wazi sana kuhusiana na sehemu husika, hasa anayohitaji
kuirekebisha lakini akasisitiza kuwa kikosi chake kipo kamili lakini kabla ya
kuingia kwenye ligi inayotarajiwa kuwa ngumu zaidi msimu ujao, anahitaji
kurekebisha sehemu kubwa kwa ajili ya mafanikio ya msimu ujao.
“Tumecheza vizuri dhidi ya Villa, hasa kwenye kipindi cha pili
lakini bado tunahitaji kufanya kitu kwa ajili ya kuhakikisha tupo vizuri zaidi
ya hapa kuelekea msimu ujao, unajua ligi siyo kitu kidogo, hasa ukiangalia
jinsi gani Tanzania inavyozingatia kwenye soka.
“Bado tuna wiki kama nne ambazo ni kama siku 28 zilizobaki pekee
kwa ajili ya kurekebisha na kuziba mapengo madogomdogo tuliyoyaona leo, lazima
tupambane kwenye maeneo tuliyobaini upungufu kabla ya Septemba 12,” alisema
Kerr.
Lakini hali hiyo pia imejitokeza kwa kocha wa viungo wa Simba,
Mserbia, Dusan Momcilovic kwa kubainisha kuwa wachezaji wake wameongeza nguvu
ya kupambana tofauti na awali kwa maana ya fiziki, lakini wapo kamili kwa 80%
pekee na si 100% kama alivyokuwa akitaka, hivyo bado ana kazi ya kumalizia
palipobaki mapema kabla ya kuanza kwa ligi.
0 COMMENTS:
Post a Comment