Sahau kuhusiana na matokeo ya jana Jumapili katika mchezo wa kirafiki kati
ya Yanga na Kimondo FC kwenye Uwanja wa Vwawa, Mbozi, Mbeya, habari ni kuwa
kiungo wa Yanga, Geofrey Mwashiuya ‘Jofu’, amekuwa akizungumzwa sana midomoni
mwa mashabiki wa Mbeya tangu aingie jijini humo.
Kiungo huyo ambaye amekuwa gumzo kutokana na uwezo wake kuwa juu,
ametua Yanga msimu huu akitokea Kimondo FC ya Mbeya, hivyo kitendo cha kurudi
nyumbani kimewafurahisha mashabiki wa soka mkoani humo na kumgeuza ‘topiki’
kutokana na kuzungumzwa sana.
Ofisa Habari wa Kimondo, Chris Kashililika, amesema, tangu Yanga
wafike Mbeya, juzi Jumamosi usiku, Mwashiuya ndiyo anatajwa sana licha ya
kikosi hicho kusheheni mastaa kibao, akiwemo Mzimbabwe, Donald Ngoma, Malimi
Busungu na Simon Msuva. Alisisitiza ujio wa Yanga umesaidia kuitangaza timu
yao.
“Ujio wa Yanga ni neema kwetu kwa sababu hata ‘publicity’ ya timu
yetu imekua kwa hizi siku chache, lakini tangu wamefika hapa Jumamosi,
Mwashiuya ndiyo amekuwa gumzo sana kuliko hata wanaoonekana mastaa zaidi Yanga.
“Wengi wanataka kuona uwezo wake akiwa na timu kubwa (Yanga) kwa
kuwa wamekuwa wakisikia na kusoma tu katika vyombo vya habari. Sasa uwepo wake
hapa Mbeya utakata kiu yao, hiyo ndiyo sababu kubwa inayowafanya wamzungumzie
sana,” alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment