October 10, 2015


Na Saleh Ally
KOCHA Jurgen Norbert Klopp, amejiunga na Livepool kwa mkataba wa miaka mitatu ambao thamani yake umeelezwa kuwa ni pauni milioni 4 (zaidi ya Sh bilioni 10.4).

Uongozi wa Klabu ya Liverpool kama ilivyo kwa mashabiki wa kikosi cha timu yao, umekuwa na ndoto za kurudia umahiri au ukubwa ule waliokuwa nao katika miaka ya 1990.

 Liverpool ndiyo kilikuwa kigogo, lakini kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa vigogo kupitia vitabu, yaani historia huku ikionekana Manchester United, Chelsea na angalau Arsenal wakiwa na nafasi ya kuzungumza zaidi kwenye Ligi Kuu England.

Ujio wa Brendan Rodgers aliyekuwa Swansea City, ulionyesha matumaini yameanza upya kabisa. Lakini bahati mbaya hilo likafanyika kwa msimu mmoja tu, baada ya kuondoka kwa Luis Suarez, msimu uliofuata mambo yamerudi palepale.

 Licha ya juhudi kubwa za Rodgers kufanya usajili wa nguvu alioamini ungekuwa msaada mkubwa kwake, mambo yakaonekana kwenda hovyo hadi uongozi wa Liverpool ulipoamua kuachana naye baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya wapinzani wao wakubwa katika Jiji la Liverpool, Everton.

Rodgers amefutwa kazi baada ya kuiongoza Liverpool katika mechi nane tu za msimu huu akiwa ameshinda tatu, sare tatu na kupoteza mbili.
Katika mechi hizo, nyumbani ameshinda mbili, ugenini moja. Sare nyumbani ni moja na ugenini ni mbili.

Pia kikosi chake kilikuwa kimepoteza mechi moja ugenini na moja nyumbani. Uongozi wa Liverpool umeona imetosha, umemuonyesha ‘mlango’ wa kutokea.

Wakati Liverpool inaachana na Rodgers, inaonekana hali halisi ilikuwa imelenga zaidi rekodi za nyuma kwa kuwa kama ni msimu huu, Rodgers hakuwa amefikia katika hali ya kutisha sana.

Katika mechi nane, kapoteza mbili tu na ana sare tatu huku akiwa ameshinda tatu. Huenda mabadiliko ya wachezaji saba kwa msimu huu, yanachangia yeye kuwa na kikosi kilichokuwa hakijapata muda wa kucheza pamoja.

 Hii ni presha kubwa kwa Klopp ambaye anaingia Liverpool ikiwa bado inabaki na matumaini ya juu sana yanayoongozwa na nia ya kutaka kuona inarejea katika kundi la magwiji, timu kubwa au zinazoheshimiwa zaidi England, Ulaya na duniani kote.

Angalia timu ambayo imepoteza mechi mbili, imeamua kuachana na kocha wake, sasa kwa kocha anayejiunga nayo, anafanya nini? Ndiyo presha anayokwenda kukutana nayo Klopp.

Klopp tayari ametambulishwa kwa mashabiki wa Liverpool, hakika bado yupo kwenye kundi la waliowekewa matumaini ya juu sana kwa kuwa wanaijua kazi yake akiwa Borussia Dortmund.

Hata hivyo, Klopp si kocha wa ‘fastafasta’ kama ilivyo kwa Jose Mourinho au Carlo Ancelotti ambao wanaweza kufanya vizuri harakaharaka kwa kusajili wachezaji wanaowataka na baada ya miaka miwili mitatu wanaondoka zao.

Klopp ni kocha mwenye mafanikio ambayo ameyapata zaidi katika timu moja ambayo ni Dortmund. Alichukua makombe sita ya ubingwa wa Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’ (2), Kombe la Ujerumani (3) na Super Cup Ujerumani mara moja.
Lakini ni kocha anayehukumiwa na muda mrefu, kocha wa aina ya Arsene Wenger au Sir. Alex Ferguson. Yaani kocha anayetakiwa kukaa kipindi fulani kabla ya kuanza kupeleka mafanikio.

Utaona Mainz ambayo ni timu yake ya kwanza aliifundisha miaka saba na akafanikiwa kuivusha hadi kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Dortmund alitua 2008 hadi 2015, hiyo ni miaka minane.

 Hii ni sehemu inayoonyesha Liverpool bado wanastahili kuwa wavumilivu kwa kuwa hii ni mara ya kwanza Klopp aliyeshika nafasi ya pili katika tuzo ya Kocha Bora wa Fifa 2013 kufundisha nje ya Ujerumani. Hivyo kwake haliwezi kuwa jambo rahisi, lazima wamvumilie.

 Liverpool wamempa Klopp mzigo, kama ule msemo wa Kiswahili “Mzigo mzito, mpe Mnyamwezi”. Lakini kama hawana uvumilivu, Mnyamwezi huyo ataweza kuuinua kweli huo mzigo? Maana wasije wakamtimua baada tu ya kuufikisha kichwani kabla hata hajapiga hatua moja kuanza kuondoka.

Kama ni uvumilivu waliushindwa kwa Rodgers, sasa ni kwa Klopp. Mashabiki wapo tayari kufanya hivyo? Kama hawataweza maana yake baada ya miaka miwili naye aondoke? Sasa ile ndoto ya Liverpool kufanya vema, kuanza kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindani wa juu itafika lini?

Kingine ni kwamba, Klopp si kila kitu, kwani hata yeye ana upungufu mwingi kama binadamu. Mifano miwili ni bora zaidi. Kwanza ni ule wa kuteremka daraja akiwa na kikosi cha Mainz, akakubali kubaki na timu yake hukohuko daraja la kwanza.

Suala la pili ni kuboronga kwa Dortmund. Licha ya kuifundisha kwa mafanikio makubwa, lakini mambo yalibadilika, hadi kufikia kupambana kujiokoa wasiteremke daraja. Bado Liverpool hawawezi kuona kuwepo kwake kila kitu kitakwenda safi.

Nyumbani, Liverpool ilifunga mabao matano na kufungwa sita. Ugenini ikafunga matatu na kufungwa manne. Ni timu iliyofunga jumla ya mabao manane na kuruhusu 10, kweli kuna tatizo.

Mechi yake ya kwanza, Klopp anaanzia ugenini dhidi ya Tottenham Hotspur, lakini matatizo makubwa mawili katika timu yoyote yakijitokeza basi iko matatizoni, kufunga machache na kuruhusu kufungwa zaidi. Hilo ndilo jambo la kwanza Mjerumani huyo anapaswa kupambana nalo, lakini bado hawezi kuwa mkombozi wa kikosi hicho, kama wachezaji watalala au uwezo wao hautawaruhusu kuisaidia Liverpool katika kipindi hiki.



                      W    D    L

Nyumbani    2      1    1

Ugenini         1      2     1



Mechi 8 ilizocheza:

Stoke City 0-1 Liverpool

Liverpool 1-0 Bournemouth

Arsenal 0-0 Liverpool

Liverpool 0-3 West Ham

Man United 3-1 Liverpool

Liverpool 1-1 Norwich

 Liverpool 3-2 Aston Villa

Everton 1-1 Liverpool



MECHI 6 MTIHANI MGUMU:

Okt 17: Tottenham (a) – Ligi Kuu

Okt 22: Rubin Kazan (h) - Ligi Kuu

Okt 25: Southampton (h) - Ligi Kuu

Okt 28: Bournemouth (h) - Capital One

Okt 31: Chelsea (a) - Ligi Kuu
Nov 5: Rubin Kazan (a) - Europa





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic