October 23, 2015


Na Saleh Ally
SIMBA wana mchezaji naitwa Pape N’daw, ni raia wa Senegal ambaye amejiunga na timu hiyo kipindi cha mwisho kabisa cha usajili.


N’daw ni mrefu hasa, ndiye mrefu kuliko wachezaji wote wa Ligi Kuu Bara. Lakini ndiye mchezaji asiye na faida hata kidogo katika ligi hiyo.

Msenegali huyo ndiye mchezaji asiye na faida hata kidogo kwa Simba wenyewe. Pia hana msaada na lolote lile kama utazungumzia kuendelea kwa soka nchini, hasa kupitia changamoto.

Umesikia taarifa zake juzi, wachezaji wa Prisons wamefanikiwa kuushitukia mchezo wake mchafu na wa kijinga ambao sasa umekwenda moja kwa moja na kushusha imani za Wanasimba ambao wamekuwa waungwana na wavumilivu hata timu yao inapoyumba.

Wachezaji wa Prisons walishituka N’daw kuwa amevaa kitu kisichkuwa cha kawaida kiunoni. Mmoja wapo alifanya kila linalowezekana na kujua Msenegali huyo alikuwa amejifunga hirizi kubwa mfano wa ‘power bank’.



Unaijua power bank, kile kifaa kinachotumika kuchaji simu, tena ya kizamani. Maana hivi karibuni kumekuwa na power bank ambazo ukubwa wake ni nafuu lakini zina uwezo mkubwa kikazi.

Tokea Simba imemsajili, ndani ya mechi sita, hakuwa amewahi kuanza katika kikosi cha kwanza hata moja. Aliyoanza amezua tafrani kwa kuonekana akiwa na hirizi kubwa sana.

Bado inatatiza, kwamba hirizi hiyo ni yake binafsi? Au alipewa ‘mzigo’ na viongozi wa Simba afanye yake na kuisaidia timu?

Swali, vipi siku ya kwanza tu apewe, au ni mtaalamu wa mambo hayo ndiyo maana katika mechi dhidi ya Yanga aliingia akiwa amevaa viatu aina ya Adidas vimechakaa kwelikweli na akasema ni zawadi ya bibi yake?

Kuna haja gani ya kuwa na mchezaji wa kimataifa ambaye haanzi kikosi cha kwanza, kapata nafasi ya kuanza anaonyesha ni mshirikina na mtu mwenye akili finyu, za kizamani asiyeweza hata kujua kwamba mazoezi kwa juhudi, nia ya kufanikiwa au kupata ushindi ndiyo chachu ya maendeleo na si ushirikina wa kuvaa hirizi!

Nilianza kusema mara nyingi sana kuhusiana na huyu N’daw ambaye anaanza kunipa hofu kuhusiana na uwezo wa Kocha Dylan Kerr ambaye amekuwa akimng’ang’ania kwamba ni mchezaji anatakayekuja kuwa msaada mkubwa kwa Simba katika siku za usoni. Najiuliza huu ndiyo msaa wake wa kuamini hirizi ili acheze vizuri?


Mchezaji yoyote ambaye anaamini hirizi atakuwa ni mjinga, mpuuzi na asiyefaa. Kama wapo, huu ni ujumbe wao. Lakini moja kwa moja umfikie N’daw ambaye anaonyesha ndiye mwendawazimu mkuu kwa kipindi hiki kutokana na ujinga anaouleta Tanzania kutoka huko Senegal.

Siamini maendeleo ya soka huko maendeleo yanatokana na ukubwa wa hirizi. Angalau angekuwa ameshikwa nayo Donald Ngoma, Hamisi Kiiza angalau tungeanzisha mjadala kutaka kujua kama kweli hirizi inaweza kumsaidia kufunga mabao mengi.

Kerr amemuondoa Maguli anayesema hajiwezi, leo anaendelea kufunga. Amemchukua N’daw ambaye sasa anaonyesha ujinga na upuuzi huku akiwa hana msaada wowote na kikosi chake.

Inawezekana viongozi wengi ndani ya Simba wakawa wanajua sana masuala ya mpira. Lakini bado kuna kila sababu wakawa na sehemu ambayo itakuwa na uamuzi wa mwisho kama ambavyo leo Yanga au Azam FC wanakwenda.

HAkuna mafanikio katika eneo lolote lile kama kila mmoja wenu atakuwa na uwezo wa kusema na kuamua. Ndiyo maana ya uongozi, kwani kama kila anayepiga kura kumchagua rais, naye angekuwa na uamuzi kama wa rais, basi hiyo nchi au klabu haiwezi kuwa maendeleo na badala yake ni mizozo kila kukicha.

Simba wanapaswa kukua, wanapaswa kukubali huyo mtumia power bank, nina maanisha N’daw huu ndiyo wakati wake mwafaka wa kufungasha virago vyake na kuondoka mara moja.

Inawezekana wako waliokuwa wakimlinda N’daw wakiwemo baadhi ya viongozi. Aibu mmeipata, maumivu mmewapa Wanasimba na sasa inatosha.




1 COMMENTS:

  1. Kama mwandishi ungerudi nyuma na kutizama maadili ya kazi yako yanakuongoza kufanya kitu gani uwezi kusema MCHEZAJI HANA FAIDA HATA KIDOGO umevuka maadili bwana salehe atakama mchezaj ana makosa..

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic