Baada ya kutolewa katika hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi, Azam FC imesema sasa inahakikisha inarejea kwenye kiwango chake na kuendelea wimbi la ushindi katika Ligi Kuu Bara.
Azam ipo kileleni mwa ligi kuu ikiwa na pointi 35 katika mechi 13 na leo inacheza na African Sports kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Timu hiyo ilitolewa katika hatua ya makundi kwenye Kombe la Mapinduzi baada ya kupata pointi mbili katika mechi tatu na kuziacha Yanga na Mtibwa Sugar zikisonga mbele.
Kocha wa Azam, Stewart Hall amesema kuwa, ameandaa mbinu za kuhakikisha timu yake inarudi katika kiwango chake baada ya kufanya vibaya katika Kombe la Mapinduzi.
Hall raia wa Uingereza alisema, baada ya kikosi chake kuboronga katika michuano hiyo, amebaini makosa yao na kuyafanyia kazi ambapo hayatajirudia katika michezo yao ya ligi kuu.
“Tumetambua wapi tulipokosea na sasa tunajiandaa kuhakikisha hatufanyi tena uzembe kwa kucheza vibaya kama tulivyofanya kwenye Kombe la Mapinduzi.
“Tayari nimeshaandaa mbinu za kuturudisha katika kiwango chetu kile ambacho tumeweza kuonyesha kwenye michezo iliyopita na naamini tutafanya vizuri,” alisema Hall.
0 COMMENTS:
Post a Comment