January 9, 2016


Na Saleh Ally
Nilishangazwa na meza aliyokuwa amekaa Mbwana Samatta katika hafla za utoaji mchezaji bora wa Afrika iliyofanyika jijini Lagos nchini Nigeria.

Meza hiyo ilikuwa na watu nane, halafu wanne kati ya sita waliokuwa wakiwania tuzo hiyo wakashinda. Wawili walikuwa ni wazazi wa Pierre Aubameyang na Abeid Pele ambaye ni baba wa Andre Ayew ambaye alishika nafasi ya tatu Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika, nyuma ya Yaya Toure na mshindi, Aubameyang.

Herve Renard aliibuka kuwa kocha bora, Mohammed Arab wa Somalia akawa kiongozi bora, Mbwana Samatta akabeba Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika wanaocheza ndani ya bara hilo. Huenda ilikuwa ni meza yenye baraka.

Baraka inafuatia baada ya juhudi, waliofika hapo wote walikuwa ni wale waliokuwa wakipambana bila ya kuchoka au kupumzika na walikuwa na ndoto ya kufanya vizuri, siku fulani.

Samatta amewatoa kimasomaso Watanzania kwa kushinda tuzo hiyo na kuweka rekodi mpya ambayo Watanzania walikuwa wakiona si jambo linalowezekana.


Kawaida Watanzania wengi hawajiamini, wanakubali kujidharau na kuamini vitu vizuri au bora hufanywa na wageni au wanaotoka nje ya Tanzania.

Samatta ameshinda tuzo ambayo miaka miwili nyuma alishinda Mohammed Aboutrika, gwiji wa Al Ahly na Misri. Maana yake sasa ni mchezaji wa kiwango hicho.

Samatta amekuwa mchezaji anayeweza kuisaidia timu kutwaa ubingwa wa Afrika. Mchezaji anayeweza kufunga mabao katika mechi mbili za fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, usisahau bado ni Mtanzania.
Hii inaonyesha Watanzania wanaweza, wana vipaji vingi, tena vya kutosha tu, lakini tatizo ni uongozi na namna ya kujiongoza.

Kabla ya kulizungumzia hilo, nieleze namna na nilivyoshangazwa kuona dunia haiiamini kabisa Tanzania. Huenda inaweza kuzidi kudidimia kwa kuwa Watanzania wenyewe hawaiamini nchi yao na vitu vyake lakini majirani nao hawaiamini kabisa.

Baada ya Samatta kushinda tuzo hiyo, alikuwa akizungumzwa kwenye mitandao kibao kutokana na ushindi wake huo ambao kwa asilimia kubwa ulitarajiwa kabisa. Angalau Kidiaba alionekana kuwa mpinzani lakini raia wa Algeria, Bounedjah Baghdad hakuwa na nafasi kwa Samatta.


Baada ya ushindi huo, kilichotokea ni vyombo mbalimbali vya habari vya Afrika Mashariki na Magharibi vikamvisha uraia wa nchi tofauti na si Tanzania ambako ni kwao. Huenda imezoeleka mara nyingi zinazofanya vizuri ni nchi za Afrika Kaskazini kwa Waarabu, Magharibi na angalau Kusini na si Mashariki.

Wikipedia ambao ni mtandao maarufu, uliamini Samatta ni raia wa DR Congo inapotokea timu ya TP Mazembe. Mtandao wa NBC wa Marekani ukaamini mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba anatokea nchini Tunisia!

Samatta si mgeni au mtu wa kutafuta historia au rekodi zake. Sasa vipi waandishi au vyombo hivyo wasijue kama kweli anatokea Tanzania? Au na wao hawaamini kama Tanzania ina uwezo wa kuwa na mtu wa namna hiyo!

Watanzania hawajiamini, hawathamini vya nyumbani kwao na hawavipendi kama vya wageni. Lakini ajabu hata wageni nao hawavijui wala kuvifuatilia na kuvikubali vitu vya Tanzania.

Huenda hili limegeuka ni utamaduni, na moja kwa moja narudi pale niliposema kuna tatizo la viongozi na kujiongoza.

Viongozi ni shida katika suala la uongozi. Utaona hata Samatta anapokelewa usiku wa manane na sherehe yake itafanyika usiku pia huku Watanzania kibao wapenda mpira wakiwa hawana nafasi ya kumuona.

Hakika nchi kwa ujumla, Serikali na TFF yenyewe hawakuwa na msaada hata nusu kwa Samatta. Sasa basi hata kupanga tu kwamba nini kifanyike ili Watanzania kwa wingi wajumuike naye, nalo limewashinda na wanaacha mambo yaende kienyeji tu.

Kawaida mpira unachezwa mchana, kama usiku basi si wa manane, maana si disko au shoo ya muziki. Watanzania walipaswa kuungana na Samatta mchana au jioni kusherehekea au kuujua angalau utamu wa tuzo hiyo inayoweza kuwa hamasa kwao. Sasa vipi TFF hata hilo imeshindwa kulifanyia kazi? Hapo ndipo ninapoanzia kwamba viongozi si makini.

Kuwa na viongozi wengi wasio makini, kumechangia soka na michezo mingine kuyumba mfululizo miaka nenda rudi. Sasa hili la Samatta lingewezekana kuwa chanzo cha wao kuona aibu na kubadilika. Mwanzo tu, wanaonekana wameshafeli, hofu yangu wataendelea kutupitisha kwenye miiba, milele.


Pili ni kwa wachezaji wenyewe, wapo wanaochipukia na wana uwezo wa kwenda mbali zaidi. Shida ni moja, wameshindwa kujiendesha. Ndiyo, nilitamani angalau mapokezi ya Samatta au sherehe zake zifanyike mchana ili na vijana nao waende, huenda sherehe hizo zikawa mwanzo wa mabadiliko yao.

Hakika hauwezi kuwa binadamu unayesubiri kusukumwa tu. Katika mahojiano na Championi, Samatta alieleza namna ambavyo amekuwa akifanya mazoezi binafsi ili kujiweka imara na safi zaidi.

Kumuangalia na kumchukulia Samatta poa tu ni sawa na kufurahia faida ya muda mchache tu. Maana tutasubiri, akistaafu itabaki hadithi na hakuna mwingine atakayesonga mbele.

Wachezaji lazima wakubali wanatakiwa kubadilika, hadithi zisiwe nyingi na kuona hakuna kinachowezekana bila ya akademi. Samatta amepitia ipi? Tunajua juhudi na kupania kutimiza ndoto kumemsaidia sana.

Basi anayetaka mafanikio, iwe kwa vitendo tena kwa kujituma. Hadithi nyingi tu na kulalama bila ya kujituma itakuwa ni kazi bure tena na tena.

Bado wengine wanaweza kupanda na kwenda mbali kupitia ndoto na kujituma kwao. Malengo ambayo kila mmoja anataka kuyafikia na ikiwezekana sherehe ya alichokifanya Samatta isiwe ya muda mrefu sana ili watu warudi kazini wakiwa na hasira, nao wakatafute njia ya kujikomboa na kuukomboa mpira na michezo mingine kwetu Tanzania.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic