March 7, 2016

YANGA

Klabu ya Yanga imepewa onyo kali kuwa itakutana na wakati mgumu kwenye mchezo dhidi ya APR ya Rwanda kutokana na aina ya soka walilonalo wapinzani wao hao.
Yanga inatarajiwa kukutana na APR kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya pili unaotarajiwa kupigwa mjini Kigali, Jumamosi ijayo.

Yanga imetinga hatua hiyo mara baada ya kuitoa timu ya Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, huku APR wakiwatoa Mbabane Swallows ya Swaziland kwa jumla ya mabao 4-1.

APR inayomilikiwa na Jeshi la Rwanda inawategemea wachezaji wake, nahodha Albert Ngabo, Iranzi Jean Claude, Yannick Mukunzi, Rwatubyaye Abdul na Bigirimana Issa ambao wamekuwa na uwezo mkubwa wa kuipa ushindi timu yao inapokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Kocha wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, Johnny McKinstry, raia wa Ireland ambaye juzi Jumamosi aliikuwepo Uwanja wa Taifa, Dar akiushuhudia mchezo kati ya Azam na Yanga, alisema kuwa kwa jinsi alivyowaona Yanga, amegundua watapata wakati mgumu sana mbele ya APR kutokana na aina ya soka lao.

Alisema kuwa kitu kikubwa kitakachowapa taabu ni jinsi APR wanavyocheza ambapo hutumia sana pasi nyingi za chini tofauti na Yanga ambao hutumia mipira ya kukimbizana.

“Licha ya kuwa nimewaona Yanga kwenye mechi moja tu lakini staili yao ya uchezaji ina utofauti mkubwa na APR, kitakachowasumbua ni kukutana na wachezaji ambao wanapiga pasi nyingi za chini ambapo kama hawatakuwa makini wataishia ‘kusafa’ tu.


“Kingine pia APR ina wachezaji wengi vijana wenye uwezo mkubwa tofauti na Yanga, lakini kama watakuwa makini na hii staili yao ya kukimbiza itawasaidia kwenye kushambulia kwa kushtukiza ‘counter attack’ kwa sababu wana washambuliaji wenye kasi,” alisema McKinstry. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic