PONDAMALI |
Kocha wa Makipa wa Yanga, Juma Pondamali, ameamua kutoongeza mkataba mwingine, baada ya ule wa awali kufikia tamati.
Pondamali alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Yanga tangu msimu wa 2014/15 ambapo amebakiza mwezi mmoja na nusu ili kukamilisha mkataba wake huo.
Pondamali, kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, amesema hatarajii kuongeza mkataba mwingine na klabu hiyo licha ya kutoufahamisha uongozi juu ya suala hilo hadi utakapomalizika na kudai kuwa anashindwa kuliendeleza kundi lake la muziki ambalo linaelekea kufa.
“Nimebakiza mwezi mmoja na nusu kukamilisha mkataba wangu wa kuitumikia Yanga lakini sijakaa chini kuzungumza na viongozi wa timu hiyo kuhusu kuongeza mkataba mwingine ama la.
“Ila kwa upande wangu sitarajii kuongeza mkataba mwingine kwa kuwa viongozi wamenipa masharti magumu ambayo yananifanya niwe mbali na kundi langu la muziki, hivyo kujikuta linakufa taratibu.
“Bado sijautaarifu uongozi juu ya adhima yangu hiyo, nasubiri pindi mkataba wangu utakapoisha rasmi ndipo niweze kuwataarifu juu ya kutoendelea kuifundisha Yanga katika msimu mwingine, naamini kuna makocha wengi wa makipa wapo watakuja kushika gurudumu.
“Lengo langu ni kutaka kujikita zaidi katika muziki ikiwa ni pamoja na kutembea mikoani kote ili kuweza kulikuza kundi kwani nikiendelea kuwa huku litakufa,” alisema Pondamali.
0 COMMENTS:
Post a Comment