November 26, 2016



Na Saleh Ally
IMEKUWA vigumu sana kuwaambia Watanzania wengi wapenda michezo kama tunaporomoka kwa kasi kubwa hasa kama utazungumzia mchezo wa soka.

Wengi wamejazwa siasa, mafundi wa siasa wamekuwa wengi michezoni na mwisho wengi wanaamini wanaoiporomosha soka ya Tanzania ni watu wema lakini wanaonewa tu.

Wengi wameaminishwa kwamba wanaokosolewa ni watu bora kabisa, lakini hawapendwi tu kutokana na juhudi zao za kuusaidia mchezo wa soka! Haya ni mawazo yaliyokandamizwa na uongo mkuu.

Uzuri wa mchezo wa soka, majibu yake mengi hupatikana kwa kutumia hesabu. Maana yake kama ulivyo mchezo wenyewe, hauchezwi chumbani au ndani ya ofisi, mwisho kila kitu kinakuwa hadharani.

Kwa sasa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wako ‘busy’ na kampeni za kuhakikisha wanarejea madarakani kupitia uchaguzi ujao. Mambo yanakwenda kimyakimya, figisu, fitina na ubabe huku wakipanga safu ya kuwapa kura.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi tayari ana uhakika wa kura kutoka Kagera ambako yeye ni mwenyekiti wa soka, maana yake watu wake hawawezi kumuangusha.

Juhudi zinaendelea kupanga watu ambao watakuwa tayari kusaidia rais huyo wa sasa aliyefeli kurejea tena madarakani. Hizi si juhudi za kusaidia mafanikio au maendeleo ya mchezo wa soka hata kidogo.

Chukua ile kauli ya “Mjenga nchi….”, lazima tukubali, “Muua soka ni mwanasoka au mpenda soka.” Ndiyo maana unaona wako wanaopambana usiku na mchana kuurudisha madarakani uongozi huu wa sasa wa TFF huku wakijua kila kitu ni shaghalabaghala.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambao ni baba wa soka, juzi wametoa takwimu zao za ubora wa viwango vya soka na kwa mara ya kwanza Tanzania inaonekana kwenye nafasi inayotia kinyaa na huzuni kubwa kwa yeyote ambaye anaupenda mchezo huo.



Tanzania iko katika nafasi ya 160, hii ni baada ya kuporomoka nafasi 16 ndani ya mwezi mmoja. Yaani kutokea Oktoba hadi Novemba 2016. Kuporomoka kwa nafasi 16 ndiyo anguko kubwa la haraka zaidi katika historia ya soka nchini ambayo ilikuwa inashikilia mafanikio makubwa ya kupanda kwa hatua hizo wakati wa Leodegar Tenga.

Tanzania kuwa katika nafasi ya 160, utaona katika Bara la Afrika inazizidi timu za Shelisheli, Djibouti, Eritrea, Gambia na Somalia. Hii hakuna ubishi tena kwamba Tanzania ni kati ya nchi za Afrika zilizo katika mstari wa nchi zilizo katika kiwango cha chini kabisa katika mchezo wa soka.

Hatuwezi kujitetea tena kwa kutumia takwimu ambazo ni hesabu na ndizo mwisho zinakuwa majibu sahihi. Lakini siasa ya maneno tunaonewa au tunajitahidi inaweza kuzungumzika.

Naweza kurudia ingawa nilisema mapema kwamba Malinzi amefeli, wako waliomtetea, huenda huu ndiyo wakati nami ningependa kuwasikia wakiinua midomo yao na kusema, wapi wanaona amefanikiwa.

Niwaase mapema wakati wakizungumza takwimu wasizungumze siasa, mfano kuhusiana na kuanzishwa kwa ligi mbili, ile ya wanawake na ile ya vijana.

Angalia maandalizi ya uanzishwaji wake umejaa haraka na papara iliyopitiliza. Hii yote ni kutaka kuwafumba macho wengi wasiojua michezo na wanaoweza kumezwa na siasa.
Ligi hizo mbili zimeanzishwa kama sehemu ya kampeni ya uchaguzi mwakani. Itaelezwa kuwa unaona sasa tuna ligi za wanawake na vijana. Utaona zimeanzishwa kwa pamoja wakati si sahihi. TFF sasa inahaha fedha za uendeshaji wakati ingeweza kuanza na moja, ikiimarika ikafuata nyingine.



Zimeanzishwa pamoja kwa haraka, kwani haraka ilikuwa ni ya nini? Yote ni kuona kila kitu kimeyumba na sasa ni bora kuwaziba midomo wanaoweza kuona kwa kuanzisha ligi hizo.

Wakati Malinzi anatambulishwa Novemba 3, 2013 na kukabidhiwa ofisi na Tenga, Tanzania ilikuwa ya 120. Baada ya mwaka mmoja ilikuwa imefika katika nafasi ya 105, huku uongozi wa Malinzi mara kwa mara ukizungumzia upandaji wa kasi katika Fifa Rank kama kigezo cha maendeleo.

Ilipoanza kuporomoka hadi leo Tanzania iko nafasi ya 160, hakuna tena kwenye uongozi huo anayetaka kuzungumzia Fifa Rank na zinaonekana tena kama si kipimo cha maendeleo ya mchezo wa soka! Ukiangalia, Sudan Kusini ambayo haina hata miaka mitano katika michuano ya soka Ukanda wa Afrika Mashariki, tena wakitawaliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, wapo katika nafasi ya 170, tofauti yao na Tanzania ni nafasi 10 tu! Haya ni maumivu makubwa kama kipimo kwa mtu aliye makini.

Kama Malinzi amekaa miaka mitatu, Tanzania imeporomoka kwa nafasi 40 za ubora. Unajaribu kujiuliza akipata nafasi hiyo kwa miaka minne ijayo maana yake hakuna ubishi kutakuwa na anguko la kishindo zaidi.

Kama Tanzania itaporomoka kwa nafasi nyingine 40, maana yake itakuwa ni ya 200. Hizo ni nafasi zinazoshikiliwa na nchi kama Somalia na Djibouti ambao ni maarufu kama vibonde. Haina shaka akibaki Malinzi, tutakuwa rasmi kama vibonde.



Unajiuliza, Fat ambayo haikuwa na wadhamini au mamilioni ya fedha kama inavyopata TFF ya Malinzi, haikutufikisha hapa, TFF ya Tenga ambayo pia haikupata wadhamini au fedha nyingi kutoka kwa wadhamini kama shirikisho chini ya Malinzi, haikutuporomosha kwa kasi kubwa ya kiwango hiki! Lakini pamoja na kuporomoka huku, kila msemakweli ni mbaya na kila mwenye maslahi yake binafsi hajali kama nchi inauawa kisoka, anachoangalia ni kumtetea ampendaye au amfaaye.

Waungwana tuwe wakweli, tuzungumze ukweli, tuache unafiki. Tuukomboe mchezo wa soka hapa nyumbani. Tayari tumeingia kwenye aibu na mwisho tutavitesa vizazi vijavyo. Serikali kama kweli inapenda maendeleo ya michezo, basi iukomboe huu wa soka, tayari upo shimoni na kilichobaki ni kushusha udongo ili kumaliza kila kitu.



NCHI ZINAZOZIDIWA NA TANZANIA KWA UBORA AFRIKA:
Shelisheli
Somalia
Djibouti
Eritrea
Gambia

TAIFA STARS
NAFASI  MWAKA    MWEZI
160       2016            Novemba
144       2016            Oktoba
132       2016            Septemba
124       2016           Agosti 
123       2016           Julai
136       2016          Juni
129       2016          Mei
130       2016         Aprili
125       2016        Machi
125       2016        Februari
126       2016        Januari   


NAFASI    MWAKA
132            2015
105            2014
120            2013


1 COMMENTS:

  1. hivi kassim dewji bado ana hasira za kukosa tenda ya vifaa vya michezo tff ya malinzi!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic