Unaweza kusema leo ndiyo Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, anaanza masomo yake kuhusiana na soka la Bongo.
Anatarajia kuanza mtihani wake wa kwanza wa mechi za kimashindano leo Jumamosi atakapoiongoza timu yake kuvaana na maafande wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza timu hizo zilipokutana, Yanga ikiwa chini ya Mholanzi, Hans van Der Pluijm, iliibuka na ushindi wa mabao 4-0, hivyo mashabiki watataka kuona jipya kutoka kwa kocha mpya Lwandamina, akiwa ameongeza wachezaji wawili, Mzambia, Justine Zulu ‘Mkata Umeme’ na Mzanzibar, Emmanuel Martin.
Yanga ikishinda mchezo huo, itakwenda kileleni japo kwa saa 24 kabla ya Simba kuvaana na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, keshokutwa Jumapili. Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 35 wakati Yanga ni ya pili ikiwa na 33.
Lwandamina, tangu atue Yanga amecheza mechi moja tu ya kirafiki dhidi ya JKU ya Zanzibar na kuambulia kichapo cha mabao 2-0 lakini alijitetea kwamba alikuwa anawajaribu wachezaji wake wote.
Mechi nyingine zinazotarajiwa kupigwa leo ni Mbeya City dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine huku timu zote zikiwa zimefanya marekebisho kwenye vikosi vyao.
Ruvu Shooting itaikaribisha Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Mabatini huku Mwadui ikiikaribisha Toto Africans katika Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
Mechi za keshokutwa ni Ndanda vs Simba, Mbao FC vs Stand United kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, African Lyon itavaana na Azam FC kwenye Uwanja wa Uhuru. Mechi hii itakumbusha ile ya raundi ya kwanza baina ya timu hizo ambayo ilikuwa kali na ya kuvutia n a iliwalazimu Azam wasubiri hadi dakika ya mwisho ya muda wa nyongeza kusawazisha bao. Iliisha kwa sare ya 1-1.
Mechi nyingine Jumapili ni kati ya Tanzania Prisons na Majimaji itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.







0 COMMENTS:
Post a Comment