March 20, 2017
Na Saleh Ally
YANGA imeshindwa kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kutokana na sare mbili mfululizo.

Sare ya kwanza ilikuwa ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam, hii ndiyo iliyoitoa Yanga baada ya sare ya bila mabao mjini Lusaka. Zanaco wamevuka kwa faida ya bao la ugenini.

Wakati Yanga inatolewa, lazima kukubali kwamba yale malengo ya kumuondoa Kocha Hans van Der Pluijm na kumchukua Mzambia, George Lwandamina yamefeli.

Yamefeli kwa kuwa kwa viwango vya Tanzania, Pluijm raia wa Uholanzi alifiti na kupata mafanikio yote. Yanga ilitaka kocha ambaye ataipeleka Ligi ya Mabingwa Afrika mbele zaidi na si kurudi katika Kombe la Shirikisho. Lakini leo wametumbukia katika shimo alilopita Pluijm, msimu uliopita.
Yanga walitaka kwenda zaidi ya pale alipoishia Pluijm katika Ligi ya Mabingwa. Hawakutaka kuangukia tena katika Kombe la Shirikisho ambalo msimu uliopita walikuwa na mafanikio kwa kiwango chao au chetu.

Pluijm alishindwa Ligi ya Mabingwa Afrika, akarejea Kombe la Shirikisho na kufanikiwa kufuzu kucheza hatua ya nane bora ambako ndiyo ulikuwa mwisho wa Yanga.

Hakika msimu uliopita kwa Yanga haukuwa haba. Pamoja na kushinda ubingwa wa Bara, Kombe la Shirikisho lakini walikwenda hadi nane bora ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza.

Kutaka zaidi si jambo baya hasa kwa mtu ambaye ni mwenye malengo. Hauwezi kuwalaumu Yanga kumleta Lwandamina kama sehemu ya kuangalia kwenda mbele zaidi kwa kuwa walikuwa katika kujaribu.

Lazima wote tukubali kwamba Yanga walikuwa na nia nzuri kwa ajili ya klabu yao. Lakini si kila unalopanga huwa lazima liwe unavyotaka kwa kuwa unakutana na watu ambao pia wanapanga na wanakuwa na malengo yao.
Katika mipangilio ya malengo unaweza kuteleza na kutoa nafasi kwa wenzako. Huenda kuna wengine waliteleza msimu uliopita na Yanga ikafanikiwa.

Lwandamina anapaswa kuelezwa ukweli kwamba amefeli lile lengo hasa la kutaka kuiona Yanga inavuka kutoka katika nane bora ya Kombe la Shirikisho hadi Nane Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini anapaswa kupewa sapoti katika Kombe la Shirikisho kwa kuwa Yanga wanapaswa kukubaliana na kilichotokea kwamba bado wanashiriki michuano ya kimataifa. Wao ndiyo wawakilishi wa mashabiki na wanachama wao na wawakilishi wa taifa la Tanzania.

Hivyo Lwandamina sasa anapaswa kuwa na plani mpya na ya uhakika kuhusiana na michuano ya Kombe la Shirikisho na si wakati mzuri kuanza kuwaza kuhusiana na walivyotolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa kifupi au hali halisi ni kwamba, Lwandamina ana deni, kwani Pluijm aliyepita kabla yake, alifanya vema na kufika hatua ya juu zaidi katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho. Hivyo kwa kuwa ameangukia huko, ni lazima kufanya juhudi na maarifa na kuhakikisha anafikia pale alipokuwa kocha huyo aliyepita na ikiwezekana kuvuka pale.
Kama kocha mzoefu na aliyepata mafanikio, lazima ajue tofauti ya Yanga na Zesco kwa kuwa Yanga ni timu ya wanachama na si timu ya kampuni. Pia ina presha kubwa sana ukilinganisha na Zesco ambayo inamilikiwa na Shirika la Umeme la Zambia.
Kingine kikubwa ni kwa mashabiki na wanachama wa Yanga wenyewe. Nao wanapaswa kujua kwamba kama alifanikiwa akiwa na Zesco, basi inawezekana na sapoti kutoka kwa wanachama au mashabiki wao wachache na viongozi, ilikuwa kubwa sana.
Hivyo, kwa kipindi hiki badala ya kuendelea kumsakama. Kuendelea kumuona kama ni mtu mbaya sana, basi iko haja ya kumuunga mkono ili aonyeshe au awape alichonacho na vizuri kama atashindwa huku wakiwa wakimuunga mkono.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV