April 10, 2017



Na Saleh Ally
YANGA wamepambana na kuifunga MC Alger kwa bao 1-0 katika mechi ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, juzi.

Mechi ilikuwa nzuri, kwa walioshuhudia waliona namna ambavyo Yanga walipambana kupata mabao na ikiwezekana zaidi ya bao moja ambalo walipata.

Yanga walijitahidi lakini hawakuwa makini hasa ukizungumzia suala la umaliziaji. Ilikuwa ni lazima kuongeza umakini ili kupata nafasi ya kufunga zaidi.

Kwa namna walivyocheza Yanga, ilionyesha wazi ni timu ambayo ilikuwa tayari kupambana na kufanya vema na huenda hili lilikuwa zuri zaidi kwa wachezaji kwa kuwa tayari kulikuwa na taarifa walikuwa na mpango wa kugoma kutokana na kucheleweshewa mshahara wao.

Lakini MC Alger imeonyesha kabisa si timu rahisi au laini, ni timu ambayo ina wachezaji wanaojitambua na wanajua wanafanya nini.

Katika mashambulizi waliyokuwa wanapeleka hatari ilikuwa inaonekana wazi. Hii ni wazi kuwa Yanga wamekutana na timu nzuri. Uzuri wake unaweza kudhihirishwa na mambo mawili tu.

Kwanza ni timu ambayo imefikia hatua hiyo na imevuka baada ya kuzifunga timu kadhaa bora. Kama isingekuwa na kiwango kizuri, maana yake isingefikia hapo ilipo.

Pili, namna ilivyocheza. MC Alger imeonyesha ilikuwa na mipango kama ambavyo zimekuwa timu nyingi za Kiarabu zilizowahi kufika na kucheza hapa nchini. Kwanza huwa ni kujilinda kwa asilimia kubwa na kufanya mashambulizi ya kushitukiza inapotakiwa.

Ndiyo maana baada ya kufungwa bao, MC Alger walifunguka na kuanza kufanya mashambulizi mfululizo angalau wakitaka hata bao moja. Lakini kikubwa walitaka sare, jambo ambalo walifeli. Hii ni wazi wakiwa kwao watakuwa na mipango tofauti na ile waliyoionyesha Uwanja wa Taifa, juzi.

Yanga wategemee mambo tofauti na wao tunaamini watakuwa nayo tofauti pia kwa kuwa wanakwenda wakiwa na bao moja na pia watakuwa wanacheza ugenini dhidi ya timu iliyo nyumbani inayotaka kusawazisha na kushinda.

Baada ya Yanga kupata ushindi wa bao 1-0, mjadala ambao umekuwa ukiendelea ni pamoja na kusema Yanga wameshatoka na safari imewakuta. Mimi naona huu si mjadala ulioshiba kwa kuwa hauna takwimu sahihi zinazoonyesha kweli Yanga wamefeli tayari.

Naona ni kama mjadala wa kuwakatisha tamaa wachezaji wa Yanga na wengi wote walio katika kikosi hicho. Acha mimi niwe tofauti kidogo nikiamini bado Yanga wana nafasi na wana uwezo wa kufanya vizuri na kuwatoa MC Alger katika michuano hiyo na hii haitakuwa mara ya kwanza wao kufanya hivyo.

Miaka mitatu iliyopita, wakati Yanga ikisafiri kwenda Cairo, Misri  kuwavaa Al Ahly ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0, gumzo lilikuwa ni kwamba Yanga itapoteza si chini ya mabao matatu. Mechi ilipigwa katika Jiji la Alexandria na hadi dakika 90 zinaisha ilikuwa Yanga imefungwa bao 1-0. Zikaongezwa dakika 30, matokeo yakabaki hayohayo.

Ikalazimika mchezo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, Yanga walipata penalti ya mwisho ya kumaliza mchezo. Bahati mbaya, Saidi Bahanuzi alikosa, mwisho Yanga wakatolewa kwa penalti na si kufungwa nne au tano kama ambavyo wengi walidhani.

Yanga hawapaswi kuaminishwa kuwa wanaweza kufungwa nne na wakakubali. Lakini mashabiki pia nao hawapaswi kuwa wenye matokeo ya kabla ya mechi tena wakijiaminisha kuwa watafungwa nne.

Yanga ndiyo watakaoamua lolote. Kukubali wapoteze kwa mabao manne au wabadili mambo na kushinda tena. Mechi inaweza kuwa rahisi kwao kwa kuwa MC Alger wakiwa nyumbani watataka ushindi na kushambulia sana.


Umakini, mipango sahihi na kuamini inawezekana inaweza kuwasaidia. Lakini wakikubali kinachozungumzwa na kuacha kitawale vichwa vyao, basi kweli wanaweza kupoteza kwa idadi kubwa na kutolewa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic