August 30, 2017




Na Saleh Ally
NINAAMINI unajua kuwa kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportPesa iliahidi kuufanyia ukarabati Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika sehemu ya kuchezea.

Ilianza kufanya hivyo wakati Everton FC ya England ilipokuja nchini kwa ziara maalum na yaliwekwa majani maalum ambayo yangefaa kukaa kwa muda fulani na baada ya hapo yalipaswa kuondolewa.

SportPesa nao wakaahidi baada ya hapo watafanya ukarabati na uwanja huo utakuwa katika kiwango bora cha kimataifa, jambo ambalo limeanza kufanyika kweli siku nne zilizopita.

Wakati ukarabati huo umeanza kufanyika, kuna jambo lililotokea na ninaona limeenda kimyakimya na linataka kupotea hivyo. Lakini mimi nimeona litakuwa ni jambo jema kulizungumzia kuliko kuliacha lipite kimyakimya tu.

Wakati mafundi wanaanza kazi ya kuuchimbua uwanja huo wa taifa katika sehemu maalum ya kuchezea ‘pitch’, walijikuta wakifukua fuvu la mwanadamu.

Lakini kuna wale waliosema kuwa lile si fuvu la mwanadamu lakini ni fuvu. Jambo ambalo mwisho linaacha jibu lilelile kwamba lililofukuliwa pale ni fuvu na wala si jambo jingine. Sasa jiulize, fuvu liwe la mwanadamu au la, limetokea wapi katikati ya uwanja?

Suala hili moja kwa moja katika hali ya kawaida, linakwenda katika zile tabia za kishirikina ambazo zimekuwa zikifanywa katika viwanja mbalimbali vya soka wakati timu za soka zikiwa zinacheza.

Hasa timu kubwa au zile maarufu mfano wa Yanga na Simba, ndizo zimekuwa zikihusishwa na masuala hayo ya ushirikina na wao hawawezi kulikwepa hili kwa kuwa wamekuwa wakifanya matendo mengi yanayoungana na ninachokizungumzia.

Mfano, unaona siku moja kabla ya mechi ya Yanga na Simba, mashabiki wao maarufu kama “Makomandoo”, wanakuwa pale wakilinda uwanja. Kila upande unaulinda mwingine usiingie uwanjani. Hapo jiulize, wanawalinda wasiingie uwanjani kwa sababu ipi?

Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 1990, hadi mipira ya kuchezea ilikuwa ikilindwa kwa madai kuwa ikiachwa hivi, upande mmoja unaweza kuitumia. Leo watu hao hawalindi mipira na mechi zinachezwa na matokeo yanapatikana!



Wakati huu mara kadhaa tumekuwa tukisikia mara wamefukia mbuzi na kadhalika. Tumesikia mengi na huenda wengi wakataka kufanya mambo hayo yaonekane ni kama stori za kwenye kahawa. Lakini baadaye wanaumbuka hivi mambo yanajitokeza kama fuvu hilo ambalo limefukuliwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Linaweza kuwa la mbuzi au kiumbe chochote, lakini jiulize aliyekwenda kulifukia alikwenda wakati upi? Wakati gani? Aliwezaje kufanya tukio hilo bila ya kuonekana au alipewa ruhusa kutoka wapi?

Tunajua uwanja huo una ulinzi, suala la kuchimba lazima isingekuwa rahisi na mambo yakafanyika kimyakimya bila ya kuonekana. Kwangu naanza kuamini mtandao wa hao wanaofanya shughuli za ushirikina, ni mkubwa na kuna watu wanawasaidia.



Pia ninakwenda katika klabu zenyewe, zimekuwa zikikataa lakini ukweli ndani yake kuna bajeti za ushirikina ambalo si jambo sahihi hata kidogo. Na inawezekana bajeti hizo ndizo zinazosaidia kupeleka mafuvu hayo kwenye uwanja.

Jiulize sisi ni watu wa karne gani na tunaweza vipi kuwa na mafanikio kama ya Italia, Ufaransa, Ujerumani, Hispania au England ambao wanafanya maendeleo bila ya ushirikina wakati sisi tunataka kufanya ushirikina ili kupata mafanikio.

Ushirikina ni miradi ya watu wachache ndani ya klabu ambao wanaingiza fedha wakiwa wanapanga kila namna ya mipango ili kuendesha maisha yao. Lakini wanajua ni mambo yaliyopitwa na wakati na wanapunguza kasi ya maendeleo na unaona baadhi ya wanachama wa klabu kubwa wasipowekewa bajeti ya ushirikina wanaanza kufanya kampeni ya kuwatoa viongozi waliopo madarakani.

Huu ndiyo wakati wa kubadilika, tuachane na mambo yasiyokuwa na msingi na lile fuvu lililopatikana Uwanja wa Taifa, ni aibu katika michezo na mpira wa Tanzania na itakuwa vizuri pia wanaohusika na uwanja huo na viwanja vingine, wakafanya kazi yao vizuri na kutoruhusu mambo kama hayo yasijirudie.




Lakini vizuri pia kupandikiza akili zenye mlengo wa kisasa na kuangalia wenzetu waliopiga hatua mfano katika Bundesliga, La Liga, EPL, Serie A na kwingine, wamepiga hatua kupitia njia au mipango ipi. Lakini si kufanya mambo yanayochangia kutuporomosha baada ya kuamini mambo yasiyo na msaada au ambayo hayawezi kukisaidia tunachokifanya katika kipindi husika. Soka ni zaidi ya kushinda uwanjani pekee, fungueni macho waungwana, dunia inatuacha tukiwa tumesinzia.

1 COMMENTS:

  1. binafsi sijui vizuri historia ya sehemu ilipo uwanja wa taifa lakini yawezekana hapo zamani watu waliwahi kuishi hapo, na kunauwezekano mkubwa tu walikufa na pengine kuzikana katika maeneo hayo au hapo awali labda kulikuwa na makaburi hapo hivyo sitaki kuamini moja kwa moja kuwa iwapo hilo lilikuwa ni fuvu la binadamu basi walioliweka hapo ni washirikina wa vilabu vyetu kongwe. japo sikatai vilabu husika kuamini katika ushirikina, nadhani siyo busara kufungia mawazo yetu kwenye ushirikina. kuhusu ulaya kutokuwa na ushirikina pia sikubaliani na wewe, swala la ushirikina ufanyika kwa siri sana inawezeka wakawa wanafanya ushirikina lakini tusijue eidha kwakuwa ushirikina wao uko more advanced au kwa kuwa ni siri. unakumbuka kombe la dunia 1998 ufaransa walikuwa wakifanya nini kabla ya kila mechi yao kuanza?!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic