September 27, 2017



Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, amesema wanawaheshimu sana vinara wa Ligi Kuu Bara kwa sasa, Mtibwa Sugar, lakini anawaandaa vijana wake kuibuka na ushindi dhidi yao huku akimtaja mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi kwenye mbinu zake.

Lwandamina raia, wa Zambia, ameyasema hayo wakati kikosi chake hicho kitakapokuwa mwenyeji wa Mtibwa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
Mtibwa ambayo kwa sasa ipo kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi kumi, huku Yanga ikishika nafasi ya tano na pointi zake nane, itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa mabao 3-1 na timu hiyo katika mchezo wa ugenini, msimu uliopita.
Akizungumzia mchezo huo pamoja na mchezaji gani wa wapinzani wao wanayemuhofia, Lwandamina amesema hakuna mchezaji wanayemuhofia, bali wanaiheshimu timu nzima ya Mtibwa, ndiyo maana hata walipocheza na Simba hakuwa anamhofia Okwi.
“Timu nyingi msimu huu zimebadilika sana, tulizocheza nazo msimu uliopita ni tofauti na hizi tunazokutana nazo msimu huu, ukiangalia ziko imara na nyingine zimepoteza wachezaji wao muhimu.
“Kwa hiyo tunakwenda kucheza na Mtibwa kama tunavyocheza na timu nyingine, tunawapa heshima zote lakini hatuwezi kuingia na akili ya kwamba tumchunge mchezaji mmoja.
“Katika falsafa yangu, sina tabia ya kuwaambia wachezaji wangu wamlinde mchezaji fulani, hata tulipocheza na Simba sikuwaambia wamchunge Emmanuel Okwi, nifanye hivyo ili iweje, kikubwa ni kuwapa morali ya kupambana na kuhakikisha hakuna kuachia nafasi kwa yeyote na naamini tutapata matokeo mazuri.
“Kama ukiwaambia wachezaji wako wamchunge mchezaji fulani, siku zote utafeli kwa sababu soka la sasa limebadilika, wengi wanatumia sana nafasi, kwa hiyo ukiwa na akili ya kumfuata mchezaji mmoja tu, basi huku kwingine unaacha nafasi ambazo wachezaji wengine wa timu pinzani wanaitumia, ni vyema kuwachunga wote na si mtu mmoja,” alisema Lwandamina.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic