November 10, 2017



NA SALEH ALLY
KAMA unakumbukwa, wakati fulani niliwahi kuandika kuhusiana na klabu ya Toto African ya Mwanza kuwa na mambo ambayo niliyaona ni ya kitoto sana.

Kwa kuwa sikuzunguka na kila jambo nililieleza kwa uwazi kabisa, ajabu sana baadhi ya viongozi wa Toto walilalamika sana na walionekana kama vile nilifanya vile kwa lengo la kuwaandama au kuwafanya waonekane hawajui mambo.

Wengi wa waliokuwa wananilaumu ni wale ambao mimi niliwaona ni wageni Toto kwa kuwa kipindi ambacho nilikuwa nikiifuatilia sana, sikuwa nimewahi kuwaona au kuwajua.

Lakini hilo kwangu halikupoteza haki yao ya kuwa viongozi au mashabiki wa klabu hiyo kongwe kutoka jijini Mwanza ambayo hakika inashindwa kuutambua ukubwa wake na imegeuka kuwa na mambo ya kitoto.

Sasa ninaweza kuthibitisha nilichokuwa nikisema siku zile na kuanisha mambo kadhaa ambayo yalisababisha mimi kuwaita kuwa wana mambo ya kitoto.

Jambo la kwanza ambalo niliwaeleza linawaponza kukosa ushirikiano kutoka kwa Wanamwanza wengi wanaopenda michezo, ni kujichagulia upande ambao hauwasaidii lolote.
Toto wamekubali kuwa ndugu au vijana au watoto wa Yanga, jambo ambalo ni hatari sana kwa maendeleo yao. Hakuna kinachowafaidisha wao zaidi ya kuifaidisha Yanga kwa kuwa ni kubwa zaidi.

Watu wa Mwanza wanaoipenda Simba wameamua kuitenga Toto kwa kuwa mashabiki wa Yanga wanasema ni ndugu zao na wale wa Toto wanakubali lakini viongozi hawaonyeshi kukerwa na hilo.

Kutokana na hali hiyo, Toto inaweza kuwa klabu inayoifaidisha Mwanza kuona ligi mbalimbali kama Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la Kwanza lakini inaongoza kupigwa vita kutokana na huo undugu usio na faida.

Lakini viongozi wa Toto wanajua kwamba wamekuwa hawabadiliki? Ndiyo maana timu yao imekuwa inapanda, msimu mmoja miwili inateremka, inakwenda kupigania kupanda ikirudi hali inakuwa vilevile.

Vipi haina viongozi wanaoweza kuifanya ikawa timu inayopambana kugombea ubingwa au kucheza michuano ya kimataifa. Kwani Toto imekosa nini kila siku iwe na maisha yasiyo na uhakika?
Sasa wanashiriki daraja la kwanza na katika timu nane za kundi C, Toto inashika mkia nyuma ya Transit Camp, Rhino Rangers, Pamba FC, JKT Oljoro, Biashara Mara, Alliance na Dodoma FC ambao ndiyo vinara.

Toto ambayo msimu uliopita ilikuwa ligi kuu, sasa inashindwa kuhimili mikiki hata ya Alliance na Biashara Mara. Au ya timu nyingine kama JKT Oljoro na Dodoma FC zilizosahaulika?

Hawa viongozi wa Toto walishindwa kuifanya timu yao ihimiliki mikiki ya Ligi Kuu Bara, sasa hawawezi kuisaidia kuhimili mikiki ya Ligi Daraja la Kwanza na kinachoonekana Toto imeingia katika ule mchezo wake wa kitoto tena.

Kama unakumbuka nilieleza namna ambavyo ilikuwa ikipanda daraja na kuteremka baada ya misimu kadhaa. Sasa iko daraja la kwanza, badala ya kuwa timu shindani kuwania kurejea ligi kuu, imeanza kupambana kuepuka kuteremka kutoka daraja la kwanza hadi Ligi Daraja la Pili! Hii ni aibu kubwa.

Najua hakuna lisilokosa maeleza kwa Watanzania lakini Toto ya Mwanza inahitaji sura na mawazo mapya kabisa na si waliopo sasa. Nina imani kama hawa wataendelea, timu hiyo itashuka daraja la pili na miaka miachache ijayo, itapotea kabisa katika sura ya mchezo wa soka.

Viongozi wenye nia ya mafanikio lazima waongozwe na ubunifu, nia ya kutimiza walichokipanga, wasiochoka au kukata tamaa. Mwendo wa Toto ni ‘rivas’, viongozi wake wanaweza kujitetea na nini hapa wakakataa kwamba wanachofanya si mambo ya kitoto kama nilivyowahi kuwaandikia?



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic