November 8, 2017








Na Saleh Ally
KELVIN Yondani si jina geni tena katika mpira wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Beki kisiki mwenye uwezo mkubwa wa unyumbulifu unapozungumzia kazi ya uhakika.

Soka ya hapa kwetu Tanzania imetawaliwa na ushabiki kwa asilimia 90, ushabiki umefunika utaalamu na watu hawakubali kuwa wakweli au kukubali ubora wa jambo au mambo kwa kuwa wanapenda zaidi kushabikia.

Lakini bado pamoja na yote hayo, ni vigumu sana kuona hata shabiki wa Simba anaweza kufungua mdomo na kusema beki wa kati wa Yanga, Yondani hana lolote au si beki bora.


Umewahi kujiuliza kuwa vipi Yondani ameendelea kuwa “mpya” kila kunapokucha? Wanakuja mabeki wa ndani na nje ya Tanzania, wanakuwa maarufu hadi wanachuja! Wanakuwa tegemeo hadi wanaonekana hawafai lakini Yondani anaendelea kubaki beki kisiki, mwenye thamani kubwa?

Unakumbuka kuhusiana na Mrisho Ngassa au Jerry Tegete ambao waling’ara wakiwa na Yondani na wamemuacha vilevile?

Sijui kama bado unakumbuka kuhusiana na wakongwe waliong’ara na Yondani kama Athumani Iddi ‘Chuji’ na wengine walioondoka na kumuacha Yondani akionekana yuleyule?


Huyu Yondani ni nani? Kwa nini yuko hivi na unakumbuka au umesahau kuwa Yondani alikuwa beki tegemeo wa Simba, kipenzi cha Wanasimba na alipoondoka alionekana atafeli na Yanga hawakuwa hawamuamini mwanzoni lakini leo ndiyo “roho” ya ulinzi ya Yanga?


Wapo wanaoamini Yondani ni “mhuni” kwa maana ya “usela”. Lakini maisha yake ni tofauti kabisa, ni mtu ambaye ameishi miaka mingi akiwapa majibu kila waliokuwa na wasiwasi naye bila kuzungumza. Majibu yake hajibizani na mtu badala yake anafanya kazi yake kwa ufasaha na ufundi wa hali ya juu kabisa.

Yondani, mtoto wa mchezaji wa zamani Patrick Yondani au baba yake mdogo Mbuyi Yondani, anaendelea kuonyesha ametokea katika familia ya mpira, mchezaji asiye na maneno mengi mdomoni badala yake vitendo uwanjani.
Waulize waliowahi kukabana na Yondani watakueleza. 


Waulize ambao wamewahi kutaka kupambana naye shughuli yake ilivyo. Ni mtu anayeijua na kuipenda kazi yake na sijui kama unakumbuka lini amekuwa akizozana na uongozi au mashabiki. Mambo yake ni kimyakimya na majibu ni uwanjani. Nakuuliza wewe, unawakumbuka wangapi wanafanya kama Yondani?

Hakika Yondani ni kati ya Watanzania wachache wanaoitimiza kazi yao bila ya maneno mengi wala mizozo. Wasiolalamika hovyo au kuhisi wanaonewa kila wakati. Mtendaji kwa vitendo na mkimya kwa maneno na ajabu si rahisi kuona akisifiwa.


Nakumbuka, Yondani aliwahi kupata tatizo kubwa na mashabiki wa Simba, alikuwa akikabana na Ngassa wa Yanga, alipogeuka kwa kasi na kuutanguliza mpira, Yondani naye aligeuka kwa kasi na kutaka kuondoka kumkimbiza Ngassa lakini aliishia kubanwa na misuli na kulala chini.

Ngassa alikimbia na kutoa pasi iliyozaa bao. Jambo hilo likatafsiriwa ni makusudi na inawezekana kudhani hivyo kama haujawahi kucheza mpira wa ushindani hata kidogo.


Leo Yondani anaendelea kufanya vizuri, kaendelea kuwa tegemeo Yanga kwa zaidi ya miaka mitano. Ameipa Yanga makombe zaidi ya matano. Ameshiriki michuano ya kimataifa kwa mafanikio makubwa zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi. Lakini anaonekana wa kawaida.

Sisi Watanzania, hasa wapenda mpira husubiri kosa moja tulaumu miezi sita. Wakati mazuri ya zaidi ya miaka mitano hayakuwahi kufurahiwa, kupongezwa na yanaweza kufutika kwa kosa la siku moja pekee.

Angalia Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alivyokuwa akisakamwa na baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao walisahau jasho, machozi na damu aliyotoa akiitumikia Yanga. Wakaanza kulalama na kumpotezea hali ya kujiamini wakilazimisha aonekane ni mzee.


Huenda hili mnasubiri kwa Yondani pia? Akosee muwe na nafasi ya kuonekana mkilaumu. Wakati hamkuwahi kuonekana hata mara moja mkisema mazuri au kumjaza moyo wa upendo na kuendelea kufanya vema kwa kuwa amekuwa akifanya hivyo.

Kumpa mwenzako moyo ni kuonyesha upendo na unajali. Lakini unatamani afanye vizuri zaidi. Kazi ya Yondani sasa inaonyesha ndiyo difenda bora wa kati kuliko wengine wote Tanzania na ameishikilia sifa hiyo kwa muda mrefu na huenda baada ya kipindi cha akina George Masatu na wenzake wa kipindi hicho, hakuna beki aliyedumu na kung’ara kwa kipindi kirefu kama Kelvin Patrick Yondani na tunapaswa kuliona hilo na kulisema badala ya kusubiri siku akikosea, ndiyo tuamke. Hongera sana Yondani, wewe ni mfano.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic