December 2, 2017



Na Saleh Ally, aliyekuwa Ujerumani
Blog ya SALEHJEMBE imefanya mahojiano ya ana kwa ana na gwiji wa soka barani Afrika, Austine Jay Jay Okocha raia wa Nigeria.

Mahojiano hayo yamefanyika nchini Ujerumani katika jijini la Koln ambalo ni namba nne kwa ukubwa kwa miji ya nchi hiyo.

Mahojiano hayo yalianza kuchapwa jana kuhusiana na mambo mbalimbali na gwiji huyo akazungumzia mambo kadhaa huku akizungumza namna Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga ilivyomkuza.

Baada ya hapo, jana makala iliishia baada ya kuulizwa swali kuhusiana na Ronaldinho ambaye alifananishwa naye na kusababisha kuzuka kwa mjadala mkubwa kwa kuwa wapo walioamini Okocha au Ronaldinho, mmoja wao alimuiga mwenzake.

Mjadala huo haujawahi kwisha kwa kuwa kila mwenye mapenzi yake aliamini tofauti kuhusiana na mwingine.
SALEHJEMBE: Ulikwenda Fenerbahce halafu ukahamia PSG ambako ulikutana na Ronaldinho ambaye imekuwa ikielezwa umekuwa ukiiga uchezaji wake jambo ambalo limezua mjadala mkubwa. Unaweza kutueleza ilikuwaje?



Okocha: (kicheko), Ronaldinho na mimi imekuwa stori ndefu sana na kila mmoja akisema lake lakini ukweli naujua mimi. Ilikuwa hivi, Ronaldinho alijiunga na PSG akiwa kijana mdogo sana. Sidhani kama kweli ningeweza kuanza kuangalia anafanya nini na mimi nikaanza kufuatisha, ingekuwa ni kitu cha ajabu sana.

SALEHJEMBE: Maana yake, aliiga kutoka kwako?
Okocha: Inawezekana kuna vitu aliiga ambalo si jambo baya katika mchezo wa soka, lakini pia watu lazima wajue kwamba Ronaldinho alitokea Brazil.

SALEHJEMBE: Alitokea Brazil ndiyo, una maanisha nini?
Okocha: Brazil wanacheza mpira unaofanana na Afrika, wanapenda mpira wa burudani zaidi badala ya ule wa moja kwa moja. Hapa naona hivi, inawezekana kuna vitu alichukua kwangu lakini kuna vitu alikuwa navyo vinavyofanana. Alikuwa ni kijana msikivu na alionyesha alikuwa anataka kujifunza na kufanya jambo fulani zuri.
  
SALEHJEMBE: Vipi kipindi hiki mmekuwa na mawasiliano hadi sasa?
Okocha: Tunawasiliana, ni mtu ambaye anapenda kuzungumza na rafiki wa zamani. Mwaka huu mwanzoni tulikuwa wote Urusi katika masuala ya Kombe la Dunia kwa kuwa tulialikwa pamoja.




SALEHJEMBE: Uchezaji wako uliwashangaza wengi, kwa mchezaji kama wewe wa Afrika kufanya vizuri kama ulivyofanya ilikuwa vigumu kujiamini kufanya hivyo?
Okocha: Ni kweli, unajua nimetokea Afrika lakini nilitamani kupata hiyo nafasi na kuitangaza Afrika zaidi na zaidi. Nilipoipata basi nilitaka kufanya kweli na kuitangaza Afrika na wachezaji wake.

Hivyo nilitaka kufikia nilichotaka, sikuwa na uoga hata kidogo na nilijiamini sana kwa kuwa nilijua mimi ndiyo mwenye uamuzi.
  
SALEHJEMBE: Uamuzi kwa namna gani?
Okocha: Kawaida aina ya uchezaji wangu kama ulifuatilia kwa karibu, ninapokuwa na mpira mimi ndiyo nakuwa mwenye uamuzi wa mwisho.
  
SALEHJEMBE: Kuna taarifa una uraia wa Uturuki na jina lako ni Muhamet Yavuz, hii imekaaje?
Okocha: (kicheko) Kweli nina uraia wa Uturuki, nimekuwa nao kwa muda mrefu hadi sasa nimeendelea kuwa raia wa Uturuki. Pasi yao ya kusafiria huwa siitumii na niliendelea kubaki na ile pasi ya kusafiria ya Nigeria ambayo nimekuwa nikiitumia.




SALEHJEMBE: Sababu ipi imefanya usiitumie wakati uliichukua?
Okocha: Hakuna maelezo mengi sana, ila…
  
KESHOKUTWA tutaendelea na makala hii na Okocha ataelezea namna alivyochukua uraia wa Uturuki na kilichosababisha yeye kukubali kufanya hivyo. USIKOSE katika SALEHJEMBE keshokutwa JUMATATU.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic