NA SALEH ALLY
SERIKALI ilishasema kuhusiana na msimamo wake kwamba inatakiwa asilimia 49 tu kwa mwekezaji mmoja mwenye nguvu kama ambavyo Mohammed Dewji ameamua kuwekeza kwenye Klabu ya Simba.
Mfanyabiashara huyo maarufu kama Mo Dewji ameshinda zabuni ya kuwekeza katika Klabu ya Simba akiwa anatoa kitita cha Sh bilioni 20.
Fedha hizo, zitamfanya uwekezaji wake uwe asilimia 50 kama ilivyotamka Klabu ya Simba ingawa serikali imekuwa ikisisitiza yeye achukue asilimia 49 na wanachama wanaobaki kuwa na asilimia 51.
Huu ni ule mfumo wa Bundesliga kule Ujerumani ambapo wanachama kwa wingi wanakuwa na nguvu ya asilimia 51 na wawekezaji wanabaki na asilimia 49 kama watagawana au atakuwepo mmoja mwenye nguvu.
Baada ya wanachama wa Simba kukutana jana na kukubaliana kumpa Mo Dewji kwa asilimia 50, inawezekana kukawa na mkanganyiko wa suala hilo na itakuwa vizuri sana kama watakutana na kulimaliza hili mapema ili kuwe na faida.
Nitaeleza kwa nini ninasema faida. Wanachama walipewa elimu kuhusiana na suala hili, lakini lazima tukubali kwamba ni jambo ambalo kuna wale watakuwa wameelewa vizuri na wengine la.
Suala la kuwa na hisa asilimia 51 kwa muwekezaji mmoja faida yake ni ipi, au wengi ndiyo wawe na asilimia 51 na kumuacha mmoja kuwa na 49, hii pia faida yake ni ipi?
Suala la kuwekeza ni zuri kabisa na hakuna ambaye anaweza kujitokeza na kulipinga. Lakini jambo zuri zaidi kuendelea kuyafanya mambo yake kuendelea kuwa wazi zaidi kama ilivyo sasa na ikiwezekana zaidi.
Kuendelea kuyafanya mambo yakawa wazi zaidi itaondoa mambo ya vificho na kutengeneza mikanganyiko kila siku zinavyokwenda na mwisho maana ya mabadiliko yenyewe ya kupata mwekezaji itapotea kabisa na kupoteza maana.
Hivyo kama serikali na Simba wanaweza kukutana na kulijadili hili suala litakuwa ni jambo la msingi zaidi kwa kuwa linahitaji ufafanuzi na kama inaangaliwa faida ya mafanikio kwa Klabu ya Simba basi kuna haja pia ya kuangaliwa kwa wanachama wa klabu hiyo ambao wamekuwa kwa siku nyingi za maisha yao.
Inawezekana hawakuitendea haki lakini inawezekana kabisa ndiyo waliofanya ikafika ilipo sasa hadi wawekezaji wametamani kuona inafikia hapa ilipo. Hivyo naweka msisitizo wa kumalizika kwa mchakato huo kukiwa na majibu kati ya serikali ambayo ina haki ya kusimamia haki ya wananchi wake na mwekezaji ambaye pia atakuwa anataka njia nzuri iliyonyooka kwa ajili ya fedha zake.
Kwa upande wa wanachama na mashabiki wa Simba, nao wanapaswa kuendelea kuelimishwa na ikiwezekana hata wao kuangalia jambo hili kama sehemu mpya wanayoingia ambayo itahitaji subira.
Hakutakuwa na mafanikio ya siku mbili au tatu baada ya Mo Dewji kuingia, hivyo lisije likawa jambo ambalo linatolewa mfano mbaya mara zote kuhusiana na kuchelewa kwa jambo au kushindikana kwake.
Uwekezaji uliopo Simba sasa ni jambo jipya katika soka la nchi yetu lakini kuna nafasi kubwa sana ya kujifunza kama wanachama wa Simba na mashabiki wataamua kufanya hivyo.
Lakini kama kutakuwa na papara, pia kuna uwezekano mkubwa wa mfumo wenye kufeli na kusababisha malalamiko makubwa au kuanza kuamini kilichotokea ni makosa makubwa.
Lazima tuanze kuamini kuwa hakutakuwa na urahisi katika kila jambo katika mfumo huo mpya na Simba watakuwa wanakwenda huku wakijifunza mambo kadhaa.
Wakati wao wanajifunza, wengine pia watakuwa wakijifunza na huenda mabadiliko waliyofanya jana ikawa njia mpya ya mabadiliko ya mpira wa Tanzania lakini lazima kuwe na nia dhabiti badala ya kusubiri kulaumu pekee pale jambo litakaposhindikana.
0 COMMENTS:
Post a Comment