Azam FC sasa imehamishia nguvu zake kwenye michuano ya Kombe la FA baada ya Ijumaa iliyopita kulazimishwa suluhu na Lipuli na kuonekana inajitoa taratibu kweye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Timu hiyo ambayo ilichukua ubingwa wa ligi hiyo msimu wa 2013/14, hivi karibuni ilikuwa ikiifukuzia kwa ukaribu Simba ambayo inaongoza ligi hiyo, lakini kwa sasa imeachwa pointi saba huku ikizidiwa na Yanga iliyopo nafasi ya pili kwa pointi mbili. Simba ina pointi 42 na Yanga 37.
Wikiendi ijayo, Azam itakuwa na mchezo wa Kombe la FA hatua ya 16 Bora dhidi ya KMC, ambapo imepanga kujizatiti zaidi kwenye michuano hiyo ili iweze kuwa bingwa na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Idd Cheche, amesema: “Matokeo yetu na Lipuli hayakuwa mazuri, kwa sasa tunaangalia namna ya kukabiliana na KMC kwenye Kombe la FA.
“Kuachwa mbali na vinara wa ligi haimaanishi kwamba ndiyo basi tena, hatuna uwezo wa kupambana nao, bali tutaendelea kupambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye mechi zijazo.
“Lakini mbali na hivyo, msimu ujao tunataka kuiwakilisha nchi kimataifa, kwa hiyo hatutakuwa tayari kuona tunaipoteza nafasi hiyo na tumejipanga kufanya kweli kwenye michuano ya FA ili tuchukue ubingwa na kuipata nafasi hiyo.”








0 COMMENTS:
Post a Comment