February 19, 2018




NA SALEH ALLY
KUMEKUWA na gumzo kubwa kuhusiana na wachezaji ambao wamekuwa majeruhi mfululizo na wamekuwa hawana msaada kwa timu zao licha ya kulipwa mamilioni ya fedha. 

Wachezaji wameendelea kukaa benchi kutokana na kuwa majeruhi na Yanga na Simba zimeendelea kuwalipa huku wakiwa hawafanyi kazi.

Mfano Yanga wao ndiyo wana tatizo kubwa kwa kuwa wachezaji watatu wa kimataifa wako nje na maisha yanaendelea huku wakiwalipa mishahara yao mikubwa na wao hawapati kitu kwa maana ya huduma.

Kadiri siku zinavyosonga mbele, tunaweza tukajifunza mambo mbalimbali kupitia kile kinachotokea kwamba kweli Yanga inahitaji huduma na wachezaji hao ni wagonjwa.

Tuliona upande wa Simba, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe yeye alimkoromea beki Shomari Kapombe.

Hans Poppe aliona Kapombe vipi haponi haraka na aliona mambo yakienda tofauti na yalivyokuwa. Tuliona hakuwa sawa, lakini ajabu siku chache baadaye Kapombe akarejea na sasa ni msaada mkubwa Simba.

Haina maana kwamba Yanga nao wawaseme akina Donald Ngoma, Thabani Kamusoko na Amissi Tambwe. Badala yake tunaweza kujifunza jambo.

Kwanza Amissi Tambwe, wakati mwingine kumekuwa na taarifa za kutaka kulazimisha kucheza kwa kukaa nje anaona kama anawaangusha Yanga.

Mara nyingi amekuwa akitaka kujaribu akiona anaweza kufanya jambo fulani akajilazimisha na mambo yakawa sawa. Umeona alirejea mara mbili tatu na mambo yamezidi kuwa magumu.

Huenda aliharibu zaidi au aliumia baada ya kulazimisha kwa kuwa alitakiwa apumzike. Lakini kuona anawaangusha wenzake linakuwa ni jambo linalomuumiza.

Tambwe kujituma na kuipenda kazi yake limekuwa ni jambo namba moja na niliwahi kumzungumzia kutokana na alivyo.

Lakini nimejifunza tena kwa Kamusoko, huenda kwa Ulaya hili jambo unaweza usilione lakini Waafrika huwa tuna upendo zaidi kwa kuwa ni asili.


Hivi karibuni, Kamusoko amerejea mazoezini na amekuwa akifanya mazoezi na wenzake ingawa yeye anafaya mazoezi ya peke yake pembeni ili arejee taratibu.

Lakini wakati akiwa majeruhi na hawezi hata kufanya mazoezi, Kamusoko alikuwa kati ya wachezaji wa Yanga wanaotokea mazoezini karibu kila siku.

Kama wangefanya mazoezi mara tano kwa wiki, angalau atajitahidi mara tatu hadi nne kuwa pamoja nao na wakati mwingine anakaa hadi mwisho wa kipindi cha mazoezi.

Kama hiyo haitoshi, Kamusoko wakati mwingine alikuwa akiwahi mazoezini hata kuliko walio wazima na wanaofanya mazoezi.

Muda mwingi aliungana na wenzake, kuwapa moyo, kuzungumza nao na hilo kwake lilikuwa ni zoezi la kawaida na lenye mwendelezo akionyesha wazi kabisa kwamba ana mapenzi na wenzake.

Kufika kwake mazoezini kulikuwa kunaonyesha kwamba yuko na wenzake na anawaunga mkono na hii inaongeza morali kwa wengine.

Hakika Kamusoko hata kama anaitia Yanga hasara kutokana na kukaa nje, lakini amekuwa mfano wa kuigwa na hasa katika suala la nidhamu.

Unapozungumzia timu, suala la upendo na kuungana ni jambo namba moja. Mnaweza msiwe bora katika vipaji vyenu au msiwe bora katika upande wa elimu lakini bado mkafanikiwa kama mtapendana na kupeana nguvu kwa lengo la kupata kile mnachoona ni sahihi.

Hakika wachezaji wengi wa Kitanzania hawana nidhamu na hili limekuwa ni tatizo kubwa. Jiulize unamjua nani akiwa majeruhi amekuwa akienda kuwaunga wenzake mkono.

Kama mimi sijawahi kumuona namuomba umfikishie salamu kwamba nampongeza na yeye ni mfano wa kuigwa. Lakini kwa wale ambao hawajawahi kufanya hivyo, lazima wajue kuwa nidhamu ndiyo mwongozo wa mafanikio bora hasa katika mapambano.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic