Kampuni ya Star Media (T) Ltd kupitia chapa yake ya StarTimes imefanya hafla fupi ya kumkutanisha muigizaji maarufu wa China Hai Qing maarufu kama Mau Dou Dou na wasanii wa Kitanzania pamoja na mashabiki wake.
Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere (NICC) na kuhudhuriwa na wasanii mbalimbali maarufu akiwemo Natasha, Yvone na Davina.
Lengo kubwa likiwa ni kutia hamasa kwa waigizaji wa ndani kukuza sanaa yao kimataifa na pia kukutana na muigizaji Hai Qing ambaye tamthiliya zake zimekonga nyoyo za watanzania kwa miaka kadhaa sasa.
Muigizaji huyo kutoka China amejizolea umaarufu nchini kupitia tamthiliya ya Mau Dou Dou na wakwe zake iliyokuwa ikirushwa na moja ya vituo vya televisheni hapa nchini.
Mbali na tamthiliya hiyo Hai Qing ameonekana katika tamthiliya ya JIKONI inayorushwa katika king’amuzi cha StarTimes kupitia chaneli ya Star Swahili. Kampuni ya StarTimes imekuwa mstari wa mbele kukuza lugha ya Kiswahili kupitia tamthiliya na filamu zilizowekewa maneno ya Kiswahili.
Mwaka jana mwishoni, StarTimes iliandaa shindano lililolenga kupata vipaji vya kuingiza sauti na kuwapatia nafasi za ajira katika kampuni hiyo, jitihada zao zimeungwa mkono na serikali ya Tanzania pamoja na Ubalozi wa China na ujio wa Mau Dou Dou ni kielelezo tosha cha utayari wa kuendeleza na kukuza tasnia ya maigizo hasa tamthiliya nchini.
Katika hafla hiyo washindi wa shindano la vipaji vya sauti mwaka jana Coletha na Bakari walipata fursa ya kuonyesha Mau Dou Dou uwezo wao wa kuigiza sauti katika tamthiya alizowahi kucheza.
0 COMMENTS:
Post a Comment